Waziri Kabudi aipongeza SUA kwa utafiti wa kipekee unaoitangaza Tanzania duniani

Na: Farida Mkongwe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Aidan Kabudi, amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kufanya tafiti za kipekee zenye mchango mkubwa katika kutatua changamoto za afya na usalama duniani, hususan matumizi ya panya waliofunzwa kugundua kifua kikuu (TB) pamoja na mabomu yaliyotegwa ardhini.

Akizungumza Agosti 8, 2026 baada ya kutembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane, Prof. Kabudi amesema Tanzania ina sababu ya kujivunia utaalamu huo unaotekelezwa kupitia SUA, akieleza kuwa ni miongoni mwa ubunifu wa kipekee unaolitangaza Taifa kimataifa na kuonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kutoa suluhisho kwa changamoto zinazokabili mataifa mbalimbali.

Prof. Kabudi amesema uwezo wa panya hao kutambua sampuli za makohozi yenye vimelea vya kifua kikuu pamoja na kugundua mabomu ya ardhini, ni teknolojia ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watu na kurejesha maeneo yaliyokuwa hatarishi katika matumizi salama ya wananchi.


“Mimi nashukuru sana kwamba nimeona nije hapa, kwa sababu Tanzania tuna vitu vingi sana vya kipekee duniani lakini vingi havifahamiki, haya tunayoyaona hapa SUA ni fahari ya Tanzania na ni mchango mkubwa wa Tanzania kwa dunia,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema ingawa Tanzania imeendelea kufurahia amani na haina changamoto kubwa ya mabomu yaliyotegwa ardhini, utaalamu unaopatikana nchini umeweza kusaidia mataifa yaliyowahi kukumbwa na vita, yakiwemo Cambodia, Msumbiji na Angola, jambo ambalo linapaswa kutangazwa zaidi ili dunia itambue mchango wa Tanzania katika kuokoa maisha na kurejesha usalama katika jamii.

“Nataka kusema kwamba, Baba wa Taifa ambaye ndiye aliyeanzisha safari ya kukifanya SUA kuwa chuo kamili, leo angekuwa hai na akaona haya ambayo SUA imewekeza katika kilimo, sayansi na utafiti, angefurahi sana,” amesema Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi amefanya ziara hiyo katika banda la SUA kwa lengo la kujionea teknolojia, tafiti na ubunifu wa kipekee ambao haupatikani katika mabanda mengine ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki, wala katika kanda nyingine nchini, huku baadhi ya bunifu hizo zikiwa za aina yake duniani.








Comments

Popular posts from this blog

SUA yabuni mfumo wa AI wa kuhesabu vifaranga vya samaki

SUA yaibuka kinara taasisi za mafunzo na utafiti Nanenane 2026

Utafiti wa SUA wabaini ongezeko la visima na changamoto za maji Dodoma