SUAMEDIA

Waziri Kabudi ataka mafanikio ya SUA yatangazwe zaidi duniani

Na: Farida Mkongwe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuongeza msukumo katika uandishi wa habari za maendeleo, sayansi, tafiti na ubunifu ili mafanikio makubwa yanayopatikana katika taasisi za Kitanzania yasibaki kufahamika ndani ya nchi pekee, bali yatangazwe na kutambulika katika mataifa mbalimbali duniani.

Prof. Kabudi ametoa wito huo Agosti 8, 2026, wakati akitembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki, ambapo alijionea tafiti, teknolojia na ubunifu mbalimbali wa kipekee unaofanywa na Chuo hicho.

Amesema Tanzania ina mafanikio mengi ya kipekee yenye mchango mkubwa kwa dunia, lakini baadhi yake bado hayajapewa nafasi ya kutosha kutangazwa, hivyo akavitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yake kuhakikisha tafiti, teknolojia na ubunifu unaofanywa na wataalamu wa Kitanzania unafahamika ndani na nje ya nchi.

Prof. Kabudi amesema mafanikio ya SUA katika matumizi ya panya hao ni moja ya mifano inayopaswa kuwa fahari ya Taifa kutokana na mchango wake katika kuokoa maisha ya watu, kuboresha uchunguzi wa kifua kikuu na kusaidia mataifa yaliyokumbwa na athari za vita kuondokana na hatari ya mabomu yaliyosalia ardhini.

Amesisitiza kuwa teknolojia na tafiti zinazofanywa na SUA hazipaswi kuishia kuoneshwa katika Maonesho ya Nanenane pekee, bali zinapaswa kutangazwa kwa nguvu ndani na nje ya nchi ili dunia ifahamu kazi kubwa inayofanywa na Chuo hicho.

Akisisitiza umuhimu wa kuzitangaza kazi za watafiti, Prof. Kabudi amesema “biashara ni matangazo,” hivyo juhudi kubwa zinazofanywa katika tafiti na ubunifu zinapaswa kwenda sambamba na mikakati madhubuti ya mawasiliano ili matokeo yake yawafikie wananchi, wadau na jumuiya ya kimataifa.

Amehimiza Chuo kuendelea kupanua shughuli hizo na kutoa taarifa mapema kuhusu hatua mbalimbali za maendeleo, ikiwemo ujenzi wa kituo kinachotarajiwa kutumika katika shughuli za sampuli za TB mkoani Arusha, ili viongozi wa kitaifa na wadau wengine waweze kushiriki, kujifunza na kuunga mkono juhudi hizo.

“Tuendelee kushirikiana, Mimi niwapongeze sana kwa utafiti huu wa aina yake ambao tunastahili kuueleza ili dunia ijue. Hii ni fahari yetu Watanzania na ni mchango wetu mkubwa kwa dunia,” amesisitiza Prof. Kabudi.






Post a Comment

0 Comments