SUAMEDIA

SUA yahamasisha ulaji wa makundi sita ya vyakula kulinda afya

Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi za Mlaji, kimetoa elimu kwa wananchi kuhusu ulaji unaofaa kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Lishe.

Akizungumza na SUA Media katika banda la SUA kwenye Maonesho ya Nanenane 2026, Bi. Khadija Boi kutoka Idara hiyo amesema ulaji wa kiafya unahitaji mtu kupata vyakula kutoka katika makundi yote sita kila siku kwa uwiano unaofaa. “Tunashauri wananchi kula kwa afya kwa kufuata makundi sita ya vyakula ili mwili upate virutubisho vinavyohitajika,” amesema.

Amesema kundi la kwanza ni la vyakula vya nafaka, viazi, muhogo na ndizi, ambalo linashauriwa kuchukua asilimia 36 ya mlo. Vyakula hivyo ni pamoja na mahindi, mtama, mchele, ulezi, ngano, muhogo, ndizi za kupika, viazi vitamu, viazi vikuu na magimbi.

Vyakula vya jamii ya kunde vinashauriwa kuchukua asilimia 18 ya mlo, vikiwemo maharage, njegere, karanga, mbaazi, kunde, njugu mawe na soya. Vyakula vya asili ya wanyama vinapaswa kuchukua asilimia 10 na vinajumuisha nyama, mayai, maziwa, samaki, dagaa, kuku na wadudu wanaoliwa kama senene na kumbikumbi.

Kwa upande mwingine, matunda yanashauriwa kuchukua asilimia 17 ya mlo na mbogamboga asilimia 17. Matunda hayo ni pamoja na maembe, ndizi mbivu, papai, mapera, machungwa, nanasi, pesheni na parachichi, huku mbogamboga zikijumuisha mchicha, kisamvu, matembele, bamia, karoti, nyanya, matango, mlenda, maboga na biringanya.

Mafuta salama yanapaswa kuchukua asilimia mbili ya mlo hivyo kuwashauri wananchi kutumia mafuta kwa kiasi na kuchagua vyanzo salama kama mafuta ya alizeti, nazi, mawese na mbegu mbalimbali zinazotoa mafuta.

Bi. Khadija amesema wananchi wanaotembelea banda hilo hupimwa uzito na urefu na kupewa ushauri wa lishe kwa kuzingatia vipimo hivyo pamoja na umri wao. Pia, banda hilo lina vifaa vya kupima kiwango cha mafuta mwilini ili kumsaidia mtu kufahamu hali yake na kupata ushauri unaoendana na mahitaji yake.

Post a Comment

0 Comments