Mwanamitandao Clemence Mwandambo avutiwa na teknolojia za SUA Mizengo Pinda

 Na: Mwandishi wetu

Mwanamitandao na mshawishi maarufu nchini, Clemence Mwandambo, ametembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Ujio wa Mwandambo katika banda hilo umeongeza hamasa kwa wananchi na wageni mbalimbali waliokuwa wakitembelea maonesho hayo, huku wengi wakijitokeza kujionea teknolojia, tafiti na huduma za kitaalamu zinazotolewa na SUA Kampasi ya Mizengo Pinda.

Miongoni mwa vivutio vilivyowavutia wananchi ni elimu kuhusu tiba inayotumia mazao ya nyuki, maarufu kama Apitherapy, ikiwemo matumizi ya sumu ya nyuki kupitia zoezi la kudungishwa nyuki chini ya usimamizi wa wataalamu.

Zoezi hilo limeendeshwa na Fundi Sanifu kutoka SUA Kampasi ya Mizengo Pinda, Bi. Juliana Maliyatabu, ambaye pamoja na wataalamu wenzake alitoa elimu kuhusu namna mazao mbalimbali ya nyuki yanavyoweza kutumika katika huduma za afya na tiba mbadala.

Wananchi waliotembelea banda hilo walipata maelezo kuhusu ufugaji wa nyuki, uvunaji wa mazao yake na umuhimu wa kupata ushauri wa wataalamu kabla ya kutumia huduma ya kudungishwa nyuki, kutokana na uwezekano wa baadhi ya watu kupata athari za mzio.

SUA Kampasi ya Mizengo Pinda, iliyopo mkoani Katavi, inaendelea kutoa elimu, kufanya tafiti na kusambaza teknolojia katika sekta za kilimo, ufugaji na hifadhi ya mazingira. Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la kampasi hiyo katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza na kupata huduma mbalimbali za kitaalamu.




Comments

Popular posts from this blog

SUA yabuni mfumo wa AI wa kuhesabu vifaranga vya samaki

SUA yaibuka kinara taasisi za mafunzo na utafiti Nanenane 2026

Utafiti wa SUA wabaini ongezeko la visima na changamoto za maji Dodoma