Na: Asifiwe Mbembela
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Copenhagen (UC) kupitia Mradi wa Biashara Endelevu ya Kaboni (SUSTCARB) wamefanya warsha yenye lengo la kujifunza kuhusu mitaala na masoko endelevu ya biashara ya kaboni.
Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii, Prof. Ernest Mauya amesema ushiriki wa wadau katika kutoa mawazo kuhusu uboreshaji wa mitaala ni muhimu katika kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika biashara ya kaboni.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa wanafunzi wanaofadhiliwa na Mradi huu unaofadhiliwa na DANIDA ili kufanya tafiti katika eneo hili la masoko ya kaboni kutasaidia kujenga uwezo kwa kitaalam na kuzalisha machapisho yatakayoweza kutoa mapendekezo ya kisera na kuchangia biashara ya kaboni yenye tija na endelevu.
Kwa upande wa washiriki, Gires Robison, Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Mafunzo ya Giografia na Mazingira SUA, Dkt. Kiwango Wilhelm wa UDOM na Prof. Thorsten Treue wa UC kwa pamoja wamesema warsha hiyo imeonyesha fursa kubwa kwa vijana kujifunza masuala ya biashara ya kaboni ambayo yanaweza kuwawezesha kujenga fursa za kiuchumi huku wakichangia katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.





0 Comments