SUAMEDIA

Utafiti wa SUA wabaini ongezeko la visima na changamoto za maji Dodoma


Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia utafiti unaochunguza mwenendo wa maji ya chini ya ardhi katika Jiji la Dodoma, kimebaini kuwa ongezeko la uchimbaji wa visima, matumizi makubwa ya maji na mabadiliko ya mazingira ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya jamii.

                                 Matokeo hayo yamewasilishwa Oktoba 16, 2026, jijini Dodoma, katika warsha ya Maabara ya Mabadiliko (Transformation Lab) chini ya Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY), unaowakutanisha watafiti, wataalamu na wadau mbalimbali kujadili changamoto zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, usimamizi wa rasilimali za maji na ustahimilivu wa jamii.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu mwenendo wa maji ya chini ya ardhi katika mazingira yenye ukame, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kutoka SUA, Brenda Mndolwa, amesema mahitaji ya maji katika Jiji la Dodoma yanaendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu na upanuzi wa shughuli za kijamii na kiuchumi. Utafiti huo umeonesha kuwa idadi ya watu katika eneo la Dodoma iliongezeka kwa takribani asilimia 86 kati ya mwaka 2012 na 2022, hali inayochangia kuongezeka kwa utegemezi wa visima binafsi na mifumo rasmi ya usambazaji wa maji.

Aidha, utafiti umebaini kuwepo kwa visima ambavyo taarifa zake hazijaingizwa kikamilifu katika mifumo ya usimamizi, jambo linaloweza kuathiri ufuatiliaji wa kiasi cha maji kinachochotwa. Matokeo yanaonesha kuwa wastani wa kina cha visima umeongezeka kwa takribani mita 86 tangu miaka ya 1950, huku visima vilivyochunguzwa vikiwa na kina cha kati ya mita 19 na 217. Hata hivyo, imebainika kuwa kuchimba kisima kirefu zaidi si lazima kuwezeshe upatikanaji wa maji mengi, hivyo kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kitaalamu kabla ya uchimbaji.

Katika eneo la mabadiliko ya tabianchi, utafiti umeonesha kuwa wastani wa mvua za mwaka katika Dodoma umeongezeka kwa takribani asilimia nane, kutoka milimita 553 katika kipindi cha mwaka 1965 hadi 1994 hadi milimita 600 katika kipindi cha mwaka 1995 hadi 2024. Pamoja na ongezeko hilo, mabadiliko ya mwenendo wa mvua, matumizi ya ardhi na mahitaji makubwa ya maji yanaendelea kuibua changamoto kuhusu uwezo wa vyanzo vya maji ya chini ya ardhi kujirejesha kwa kiwango endelevu.
Vilevile, matokeo yameonesha kuwa mwaka 2016, baada ya kupanuliwa kwa uwezo wa miundombinu ya kusafirisha maji, kiwango cha uchotaji katika maeneo ya visima kiliongezeka kutoka takribani mita za ujazo 30,000 hadi 61,500 kwa siku. Utafiti umebaini pia dalili za kushuka kwa viwango vya maji kwa kasi zaidi katika baadhi ya vipindi vya miaka ya karibuni, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na usimamizi wa matumizi ya maji ya chini ya ardhi.
Katika kufanikisha utafiti huo, watafiti wametumia mifumo ya kisayansi ya kuiga mwenendo wa maji, ikiwemo modeli ya DRYP inayotumika kuchambua mgawanyo wa maji katika maeneo yenye ukame, ili kuchunguza uhusiano kati ya mvua, hali ya udongo, matumizi ya ardhi na uchotaji wa maji katika kiwango cha maji yanayoingia na kuhifadhiwa chini ya ardhi. Kupitia warsha hiyo ya T-Lab, mradi wa CLARITY unatoa fursa kwa watafiti na wadau kubadilishana uzoefu, kujadili matokeo ya tafiti na kupendekeza hatua zinazoweza kusaidia kukabiliana na changamoto za usimamizi wa maji.

Kwa ujumla, matokeo ya utafiti huo yameonesha umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa visima, matumizi ya taarifa za kisayansi katika mipango ya maendeleo, ufuatiliaji wa uchotaji wa maji na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda rasilimali za maji ya chini ya ardhi. Hatua hizo zinatajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linaendelea kuwa na upatikanaji wa maji wa uhakika na endelevu licha ya ongezeko la watu, mahitaji ya maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.








PICHA NA TATYANA CELESTINE. ZAIDI BOFYA LINK HAPA CHINI

Post a Comment

0 Comments