Wanafunzi Mafiga waonesha mbegu bora za mpunga na mbinu rafiki za kudhibiti panya
Na: Farida Mkongwe
Mbegu bora za mpunga pamoja na mbinu rafiki kwa mazingira za
kudhibiti panya ni miongoni mwa teknolojia zinazooneshwa na Shule ya Sekondari
Mafiga katika Maonesho ya Nanenane.
Akizungumza na SUA Media katika maonesho hayo, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika mkondo wa amali, Stella Emmanuel, amesema teknolojia hizo zinalenga kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kupunguza uharibifu wa mazao mashambani.
Stella amesema miongoni mwa mbegu zinazooneshwa ni aina ya
Mwangaza na Supa BC. Ameeleza kuwa mbegu ya Mwangaza ina uwezo wa kuvumilia
ukame na kutoa mavuno mengi, hivyo kuwafaa wakulima wanaolima katika maeneo
yenye upungufu wa mvua.
Ameongeza kuwa mbegu ya Supa BC inafaa kupandwa katika maeneo yenye maji mengi kwa kuwa ina uwezo wa kustahimili hali ya mafuriko. Sifa hiyo inawapa wakulima nafasi ya kupata mavuno mazuri hata katika maeneo yanayokumbwa na maji mengi.
Mbali na mbegu hizo, wanafunzi hao wanaonesha mbinu ya asili
ya kudhibiti panya inayojulikana kama Trap Barrier System, mbinu ambayo hutumia
nailoni kuzungushia eneo la mpunga ili kuzuia panya wasiingie shambani na
kuwaelekeza katika mitego maalumu.
Stella amesema pia matumizi ya ndege aina ya bundi ni njia rafiki kwa mazingira ya kudhibiti panya, kwa kuwa bundi ana uwezo mkubwa wa kuona wakati wa usiku na kuwala panya wanaoingia mashambani na hivyo kusaidia kupunguza matumizi ya viuatilifu na kemikali zenye sumu ambazo zinaweza kuathiri mazingira na afya ya binadamu.
Comments
Post a Comment