Mwenyekiti wa Baraza la SUA ahimiza tafiti na bunifu kuwafikia wananchi zaidi

 Na: Ayoub Mwigune

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Bw. Andrew William Massawe, ametembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2026, ambapo amejionea tafiti, teknolojia na bunifu mbalimbali zinazowasilishwa na Chuo kwa wananchi na wadau wa sekta ya kilimo.

Katika ziara hiyo, Bw. Massawe amepokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa SUA kuhusu tafiti, teknolojia na bunifu zinazolenga kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wadau wengine wa sekta ya kilimo.

Baada ya kutembelea banda hilo, Bw. Massawe amewapongeza wafanyakazi na wataalamu wa SUA wanaoshiriki katika Maonesho ya Nanenane kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwafikishia wananchi elimu, teknolojia na matokeo ya tafiti zinazofanywa na Chuo.

Amesisitiza umuhimu wa juhudi hizo kuendelea hata baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Nanenane, huku akiitaka SUA kuongeza wigo wa kuwafikia wananchi ili tafiti na bunifu zinazozalishwa na Chuo zitumike zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

Amesema ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa kupitia tafiti za SUA yanawafikia wananchi wengi zaidi na kuleta matokeo chanya katika shughuli zao za uzalishaji na maendeleo kwa ujumla.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amewapongeza wafanyakazi na wataalamu wa Chuo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Maonesho ya Nanenane, akieleza kuwa juhudi zao zimeendelea kuitangaza SUA kupitia tafiti, teknolojia na bunifu zinazowasilishwa kwa wananchi.

Prof. Chibunda amewataka kuendelea kuongeza juhudi na kuboresha zaidi utoaji wa elimu na huduma kwa wananchi, ili kuhakikisha SUA inaendelea kutoa mchango mkubwa kupitia Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki na kuwafikia wadau wengi zaidi kwa matokeo ya tafiti na teknolojia za Chuo.

Amesema ushiriki wa SUA katika maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuonesha shughuli zinazofanywa na Chuo, hivyo wataalamu wanapaswa kuendelea kutoa elimu na huduma bora kwa wananchi, sambamba na kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri na wadau mbalimbali.








Comments

Popular posts from this blog

SUA yabuni mfumo wa AI wa kuhesabu vifaranga vya samaki

SUA yaibuka kinara taasisi za mafunzo na utafiti Nanenane 2026

Utafiti wa SUA wabaini ongezeko la visima na changamoto za maji Dodoma