Na: Ngolo Mboje
Wananchi wamehimizwa kutumia huduma za Kiwanda cha
Uchakataji Mbao cha Vuyisile Min
Furniture Factory, kilichopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA), kutokana na uwezo wake wa kuongeza thamani ya mazao ya misitu kupitia
matumizi ya teknolojia za kisasa.
Akizungumza na SUA Media, Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za Mazao ya Misitu, Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii Mbonea Joshua, amesema kiwanda hicho ni nyenzo muhimu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa zinazotokana na miti na mbao.
Amesema kiwanda hicho kinatumia mashine za kisasa, ikiwemo Circular Saw kwa ajili ya kukatia mbao
na Multiblade Saw kwa ajili ya
kuchana mbao, ambazo hurahisisha kazi na kuongeza ufanisi katika uchakataji wa
mazao ya misitu.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kina tanuru la kukaushia mbao
laini na ngumu, ambalo huondoa unyevunyevu kwenye mbao mbichi na kuzifanya
zidumu kwa muda mrefu kwa kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na wadudu
pamoja na changamoto nyingine zinazotokana na unyevunyevu.
Joshua amesema kiwanda hicho pia kina mchango mkubwa katika shughuli za utafiti kwa kutengeneza sampuli za maabara zinazotumika katika tafiti mbalimbali, zikiwemo zinazohusu vifaa na mitambo. Ameeleza kuwa tafiti hizo zimechangia kupatikana kwa machapisho ya kisayansi yanayosaidia jamii kupata uelewa kuhusu matumizi bora ya teknolojia za uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya misitu.
Aidha, amesema kiwanda hicho ni kituo muhimu cha mafunzo kwa
vitendo kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu, hususan
wanaosomea Sayansi ya Misitu pamoja na Sayansi ya Teknolojia ya Mbao na
Uongezaji Thamani. Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi hupata ujuzi wa kuchakata
mazao ya misitu kuanzia gogo hadi bidhaa ya mwisho yenye thamani.
Bw. Joshua amewakaribisha wananchi kutembelea na kutumia
huduma zinazotolewa na kiwanda hicho, akieleza kuwa shughuli zake zinafanyika
kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.


0 Comments