SUAMEDIA

Mhitimu wa SUA abuni mashine kurahisisha shughuli za kilimo

 Na: Ngolo Mboje

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Bw. Joshua Felix, ametengeneza mashine ya kutengeneza matuta (Ridger Machine) yenye uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kilimo, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya nguvu za binadamu na wanyama pamoja na kurahisisha kazi kwa wakulima, hususan wakulima wadogo.

Akizungumza na SUA Media, Bw. Felix, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Kilimo kutoka SUA, amesema wazo la kutengeneza mashine hiyo limetokana na changamoto zinazowakabili wakulima wanaotumia nguvu kazi kubwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali mashambani.

Amesema mashine hiyo imelenga kusaidia kubadilisha mfumo wa kilimo kutoka kwenye utegemezi mkubwa wa nguvu za binadamu na wanyama kwenda kwenye matumizi ya teknolojia, hatua ambayo inaweza kuongeza ufanisi wa uzalishaji huku ikipunguza muda na nguvu zinazotumika kufanya kazi shambani.

“Lengo la kutengeneza mashine hii ni kubadilisha mfumo wa kilimo kutoka kwenye matumizi ya nguvu za wanyama na binadamu na kuwasaidia wakulima wadogo,” amesema Bw. Felix, akiongeza kuwa mashine hiyo inaweza kutumika kulima, kutengeneza matuta, kupalilia na kufyeka, hivyo kumwezesha mkulima kufanya shughuli nyingi kwa kutumia mashine moja.

Ameeleza kuwa matumizi ya mashine hiyo yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa muda unaotumika katika shughuli za kilimo, ambapo kwa mujibu wake, inaweza kupunguza muda wa kufanya kazi shambani kwa hadi asilimia 90 ikilinganishwa na matumizi ya jembe la mkono.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa SUA, Bw. Leonard Mwankemwa, amesema Chuo kinaendelea kuwapatia wanafunzi mafunzo ya vitendo yanayowawezesha kutumia maarifa wanayopata darasani kubuni na kutengeneza teknolojia mbalimbali chini ya usimamizi wa wataalamu, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kutatua changamoto za jamii, kujiajiri na kutumia taaluma zao katika kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo.



Post a Comment

0 Comments