Na: Ngolo Mboje
Wanafunzi wa kimataifa wametakiwa kuzifahamu taratibu za
udahili na huduma mbalimbali zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA), ili kuwawezesha kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Akizungumza na SUA Media, Mlezi wa Wanafunzi kutoka Idara ya Umataifishaji na Majalisi SUA, Bw. Ogelloh Evance Obunga, amesema idara hiyo ina jukumu la kuwasaidia wanafunzi wa kimataifa katika hatua mbalimbali za udahili na usajili, pamoja na kuwapokea na kuwapa mwongozo wanapowasili chuoni.
Amesema SUA pia inashirikiana na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa
Morogoro kuwasaidia wanafunzi wa kimataifa kuomba vibali vya kuishi nchini kwa
ajili ya masomo. Aidha, ofisi hiyo huwasaidia kutumia mfumo wa maombi ya vibali
na kuwaelekeza kuhusu nyaraka na masharti yanayohitajika ili kukamilisha
mchakato huo.
Bw. Obunga amesema chuo pia hutoa msaada katika mchakato wa uthibitishaji na ulinganifu wa vyeti vya wanafunzi wa kimataifa kupitia ushirikiano na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), huku ofisi ikiratibu namna ya kuvipata baada ya mchakato huo kukamilika.
Ameongeza kuwa SUA huwasaidia wanafunzi wa ndani na wa
kimataifa kutafuta fursa mbalimbali za ufadhili wa masomo, sambamba na kuandaa
shughuli za kubadilishana tamaduni zinazowaleta pamoja wanafunzi kutoka mataifa
mbalimbali. Pia chuo kinaendelea kuwaunga mkono wanafunzi na wahitimu wake kwa
kuimarisha mitandao na ushirikiano unaowezesha kuanzishwa kwa miradi mbalimbali
ya maendeleo.
Bw. Obunga amewakaribisha wanafunzi, hususan wanaotoka mataifa ya nje, kujiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na kutembelea banda la SUA ili kupata taarifa sahihi kuhusu taratibu za udahili na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wanafunzi wa ndani na wa kimataifa.

0 Comments