Na: Ayoub Mwigune
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kimekabidhi meza tatu na viti vinane kwa Kituo cha Polisi cha SUA, ikiwa ni
sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha utoaji wa huduma
za kiusalama ndani ya Chuo na maeneo jirani.
Akikabidhi samani hizo kwa niaba ya Menejimenti ya Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala), Prof. Amandus Muhairwa, amesema ushirikiano kati ya SUA na Kituo cha Polisi cha SUA ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa watu na mali.
Prof. Muhairwa amesema Chuo kitaendelea
kushirikiana kwa karibu na kituo hicho pamoja na kutoa msaada pale mahitaji
yanapojitokeza, kwa kuzingatia uwezo, utaalamu na rasilimali zilizopo SUA.
Ameeleza kuwa SUA ina uwezo wa kutengeneza na kukarabati samani kupitia Kiwanda cha Vuyisile Mini Furniture Factory, kilichopo Kampasi ya Solomon Mahlangu, Mazimbu mkoani Morogoro hivyo amekihimiza kituo hicho kuendelea kuwasiliana na Chuo kinapohitaji msaada unaoweza kutolewa kupitia kiwanda hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Morogoro (OCD), SSP Oscar Ngumbulu, ameishukuru SUA kwa msaada huo, akisema
umetolewa wakati muafaka kutokana na changamoto ya uhaba wa samani iliyokuwa
ikikabili kituo hicho.
SSP Ngumbulu amesema meza na viti vilivyokabidhiwa vitaboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa askari Polisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Ameongeza kuwa Kituo cha Polisi cha SUA
kinatoa huduma za kiusalama kwa wanafunzi, wafanyakazi na jamii inayozunguka
Chuo, pamoja na wananchi wengine wanaofika kituoni kupata huduma mbalimbali.
Aidha, ameahidi kuwa samani hizo zitatunzwa na kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na uongozi wa SUA katika kuimarisha usalama ndani ya Chuo na maeneo jirani.






0 Comments