Huduma za mtandao za SUA zaongeza ufanisi Nanenane 2026
Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Idara ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kinatoa huduma za mtandao kwa
wafanyakazi wake wanaoshiriki katika Maonesho ya Nanenane ili kuwawezesha
kutekeleza majukumu mbalimbali ya kielimu, kiutawala na mawasiliano.
Akizungumza na SUA Media katika maonesho hayo, Msimamizi wa Huduma za Mtandao wa Intaneti katika Idara ya TEHAMA ya SUA, Kundasen Justin Swai, amesema huduma hiyo imewekwa ili kuhakikisha wafanyakazi wa chuo wanapata mtandao wa uhakika wakati wa kutekeleza majukumu yao katika banda la SUA.
Amesema huduma hiyo inaviwezesha vitengo na idara mbalimbali
za chuo kutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa njia za kidijitali, kufikia
taarifa muhimu za chuo na kuendelea kutekeleza kazi za kiofisi wakiwa katika
viwanja vya Maonesho ya Nanenane.
“Mtandao huu pia unawasaidia wafanyakazi wanaohusika na udahili kutoa taarifa na huduma kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na SUA, ikiwemo kuwaelekeza kuhusu programu mbalimbali za masomo zinazotolewa na chuo,” amesema Swai.
Aidha, amesema SUA inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi
sahihi ya mtandao na kompyuta kutokana na umuhimu wa teknolojia katika
utekelezaji wa shughuli za kila siku.


Comments
Post a Comment