Na: Farida Mkongwe
Wakulima wamehimizwa kutumia Ghala la Mkulima linalosimamiwa
na Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Sokoine (SNAL), iliyopo katika Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA), ili kupata maarifa, ujuzi na teknolojia mbalimbali
zitakazowasaidia kuongeza tija na faida katika shughuli zao za uzalishaji.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Kitengo cha Maarifa na Huduma za Rejea katika maktaba hiyo, Bw. Jabir Jabir, kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika Kanda ya Mashariki, mkoani Morogoro.
Amesema kilimo bora na chenye matokeo kinapaswa kufanyika
kwa kuzingatia taarifa na maarifa sahihi kutoka kwa wataalamu.
Bw. Jabir amesema SNAL ina machapisho mbalimbali ambayo
wakulima wanaweza kuyasoma kwa kufika maktabani au kuyapata kwa njia ya mtandao
kupitia simu janja na vifaa vingine vya kidijitali.
“Kupitia Ghala la Mkulima, wananchi wanaweza kupata taarifa,
maarifa na mafunzo mbalimbali ya kilimo
yaliyoandaliwa na wataalamu waliobobea katika sekta hiyo.
Ameeleza kuwa maktaba hiyo inawahudumia watu wa kada na viwango vyote vya elimu, huku machapisho yaliyopo katika Ghala la Mkulima yakiwa yameandikwa kwa lugha rahisi inayomwezesha mkulima kuelewa na kutumia maarifa hayo katika shughuli zake.
Amesisitiza kuwa matumizi ya taarifa na maarifa sahihi
yatawasaidia wakulima kutambua mahitaji ya soko, kuchagua teknolojia bora na
kuzalisha kwa tija.
Amesema hatua hiyo inaunga mkono kaulimbiu ya Maonesho ya
Nanenane ya mwaka 2026 isemayo, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira
2050.”
0 Comments