SUAMEDIA

Serikali yatenga Sh bilioni 9.2 kuwalipa fidia wananchi 962 wa Mindu

 Na: Farida Mkongwe

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Serikali imetenga Sh bilioni 9.2 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 962 ambao maeneo yao yanatwaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu kwa kimo cha mita 2.5, ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma za maji katika Manispaa ya Morogoro.

Malima aliwahakikishia wananchi hao Agosti 31, 2026 baada ya hafla ya utiaji saini mkataba wa kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu kwa kimo cha mita 2.5 na mkandarasi, Kampuni ya Sinohydro Corporation kutoka China ambao unatarajiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi mwaka 2028.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inawahakikishia wananchi hao ambao wametambuliwa na kustahili kulipwa fidia ili kupisha ujenzi huo kuwa watalipwa, kwa kuwa tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya zoezi hilo.

“Nimeshawasiliana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ili awasiliane na Waziri wa Fedha kwa ajili ya upatikanaji wa fedha hizo, ziweze kulipwa fidia ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa,” alisema Malima.

Mbali na hayo, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Morogoro na wanaoishi kandokando ya Bwawa la Mindu kutunza mazingira, huku akimwagiza Ofisa Madini wa Mkoa wa Morogoro kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Mindu ili kulinda mazingira ya bwawa hilo.

Mkuu wa Mkoa pia amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo ndani ya muda wa mkataba wa miezi 18 ili kukidhi mahitaji makubwa ya maji kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro.

Post a Comment

0 Comments