Na: Farida Mkongwe
Wakulima na wananchi kwa ujumla wamehimizwa kuandaa mashamba
mapema, kupanda mazao ya muda mfupi na kufuatilia taarifa zinazotolewa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kupunguza athari zinazoweza
kusababishwa na mvua nyingi za El Niño.
Wito huo umetolewa na Bi. Editha Njau kutoka Kitengo cha Ghala la Mkulima katika Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Sokoine (SNAL), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati akizungumza na SUA FM 101.1 kupitia kipindi cha Darasa Shirikishi.
Bi. Editha amesema Ghala la Mkulima lina machapisho
mbalimbali yanayohusu kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara na lishe, ambayo
wananchi wanaweza kuyapata popote walipo kwa kutumia simu janja.
Ameeleza kuwa taarifa kuhusu El Niño zimewekwa katika ghala hilo kwa lugha rahisi ili kuwasaidia wakulima kuelewa mabadiliko ya hali ya hewa, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi, mazao yanayofaa kulimwa pamoja na athari zinazoweza kujitokeza.
Amesema wakulima wanapaswa kuandaa mashamba yao mapema kabla ya kuanza kwa mvua za Novemba hadi Desemba, huku wakizingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo na hali ya hewa.
“Mvua nyingi zinaweza kusababisha maji kutuama na ardhi kubaki na unyevu kwa muda mrefu, hivyyo tunawashauri wakulima kutengeneza matuta na mitaro ili kurahisisha uondoaji wa maji na kuzuia kuoza kwa mizizi ya mimea,” amesema Bi. Editha.
Aidha, amewashauri wakulima kuepuka kupanda mazao katika mabonde na maeneo yanayopitisha maji mengi. Inapowezekana, wachague maeneo yenye mwinuko kidogo ili kupunguza athari za mafuriko na mmomonyoko wa udongo, ambazo zinaweza kusomba mbegu na kuharibu mazao mashambani.
Bi. Editha amependekeza ulimaji wa mazao yanayoweza
kustahimili mvua nyingi na ardhi yenye unyevu, yakiwemo ndizi, mihogo, viazi
vitamu, mpunga na miwa. Kwa maharage na mahindi, wakulima wamehimizwa kuchagua
mbegu za muda mfupi, zikiwemo zinazokomaa ndani ya siku 75, pamoja na kulima
mboga kama bamia na matembele.
Pia amewashauri wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha na
kufuatilia mara kwa mara taarifa zinazotolewa na TMA ili kufanya maamuzi sahihi
kuhusu shughuli za kilimo badala ya kutegemea makadirio yasiyo ya kitaalamu.




0 Comments