SUAMEDIA

Teknolojia ya Maabara Tembezi yafikisha huduma za uchunguzi karibu na wananchi

 Na: Farida Mkongwe

Maabara Tembezi ya Jenomiki (Mobile Genomic Laboratory) ya Taasisi ya SACIDS ya Afya Moja (SACIDS Foundation for One Health) imekuwa miongoni mwa teknolojia zilizovutia wananchi na wageni waliotembelea Maonesho ya Nanenane 2026, kutokana na uwezo wake wa kufikisha huduma za kisasa za uchunguzi wa vimelea katika maeneo yenye viashiria vya milipuko ya magonjwa.

Akitoa maelezo ya teknolojia hiyo inayoratibiwa na Dkt. Edson Kinimi, Mhadhiri kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa niaba ya Prof. Gerald Misinzo, amesema kwa zaidi ya muongo mmoja, taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti zinazozingatia dhana ya Afya Moja kwa kuwakutanisha wataalamu wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, mazingira na teknolojia.

Tofauti na utaratibu wa kawaida wa kusafirisha sampuli kwa umbali mrefu hadi katika maabara kuu, Maabara Tembezi ya Jenomiki hupelekwa moja kwa moja katika eneo lenye viashiria vya mlipuko wa ugonjwa, hatua ambayo hupunguza muda wa kupata majibu ya vipimo kutoka siku kadhaa hadi saa chache na kuwezesha mamlaka kuchukua hatua za haraka za kulinda afya ya umma.

Maabara hiyo imeunganishwa na mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, ikiwemo AfyaData na Afya Msafiri, pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa majanga na dharura za kiafya. Mifumo hiyo hupokea taarifa kutoka kwa jamii na vituo vya afya, kuzichambua na kusaidia kutoa tahadhari ya mapema kuhusu uwezekano wa kutokea kwa milipuko.

Dkt. Kinimi amesema teknolojia hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama wa afya, hasa kutokana na magonjwa mengi yanayoibuka kuwa ya zoonotiki, ambayo huambukizwa kati ya wanyama na binadamu. Mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na mwingiliano kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori vimeendelea kuongeza hatari ya kuibuka na kusambaa kwa magonjwa hayo.

Kupitia maabara hiyo, SACIDS imechangia katika ufuatiliaji na uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, yakiwemo Marburg, UVIKO-19, Mpox, Dengue, Chikungunya, Homa ya Bonde la Ufa, Leptospirosis, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo pamoja na Homa ya Nguruwe . Pia hutumika kufuatilia usalama wa chanjo na kutoa ushahidi wa kisayansi unaosaidia Serikali kufanya maamuzi ya kudhibiti milipuko.

Popo wana mchango mkubwa katika uchavushaji wa mimea, usambazaji wa mbegu, urejeshaji wa misitu na udhibiti wa wadudu waharibifu wa mazao pamoja na mbu, hivyo kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia.

Kwa sasa, SACIDS inaendelea na utafiti wa kubaini maeneo yenye hatari ya maambukizi ya virusi vya Marburg katika popo aina ya Egyptian fruit bats mkoani Kagera, huku ikitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuishi na popo kwa usalama na umuhimu wa kuwahifadhi. Kupitia Maonesho ya Nanenane 2026, wananchi, watafiti na viongozi wamepata fursa ya kujionea namna teknolojia hiyo inavyolinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira.



Post a Comment

0 Comments