SUAMEDIA

Bilioni 32.7 kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu, kuongeza hifadhi ya maji

 Na: Farida Mkongwe

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira baada ya kupata awamu ya pili ya fedha kutoka Serikali Kuu pamoja na mkopo wa masharti nafuu kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kiasi cha Sh bilioni 32.7.

Fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu kwa kimo cha mita 2.5, ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma za maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro na kuwezesha shughuli nyingine za uwekezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, CPA Sais Kyejo, amesema hayo katika taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu kwa kimo cha mita 2.5. Mkataba huo umesainiwa na mkandarasi, Kampuni ya Sinohydro Corporation kutoka China, na unatarajiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi mwaka 2028.

Kyejo amesema lengo la utekelezaji wa mradi huo ni kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji katika Bwawa la Mindu kutoka lita bilioni 12.62 za sasa hadi kufikia lita bilioni 22.06 baada ya kukamilika kwa mradi.

Amesema kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kunyanyua njia ya kutolea maji ya ziada (spillway) kwa kimo cha mita 2.5 na yenye urefu wa mita 100, pamoja na kunyanyua tuta la kuhifadhia maji kwa kimo cha mita 2.5. Hatua hiyo itafanya kimo cha tuta kuongezeka kutoka mita 8.5 hadi mita 11 baada ya kukamilika kwa mradi.

Kyejo amezitaja kazi nyingine kuwa ni ufungaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufuatilia usalama wa bwawa, ufungaji wa vifaa vya kisasa vya kufuatilia ubora wa maji, pamoja na ujenzi wa jengo kwa ajili ya wataalamu watakaokuwa wakihudumia bwawa hilo.

“Baada ya kukamilika kwa mradi, kutakuwa na ongezeko la maji yanayohifadhiwa katika bwawa hili, jambo litakalowezesha kuwepo kwa uhakika na usalama wa maji katika Manispaa ya Morogoro. Mradi huu pia ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kama inavyoelekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Kyejo.

Amesema upanuzi wa Bwawa la Mindu utawezesha kuongezwa kwa mitambo miwili ya uzalishaji na utibuji wa maji katika eneo la Mafiga–SUA na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 27 kwa siku hadi lita milioni 108 kwa siku.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya MORUWASA, Prof. Moses Warioba, alisema upanuzi wa bwawa hilo utaboresha huduma za maji. Alisema Bodi hiyo, kupitia Menejimenti, itaendelea kubuni njia mbalimbali za kupanua huduma za maji ili ziweze kuendana na ongezeko la watu.

AFD imetenga Euro milioni 84, sawa na Sh. bilioni 220 za Kitanzania kwa kutumia kiwango cha ubadilishaji wa fedha cha mwaka 2020, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu huku Serikali nayo ikitenga Euro milioni 14, sawa na Sh. bilioni 36.8, zinazotolewa kwa awamu kwa ajili ya kuboresha miradi ya maji katika Manispaa ya Morogoro, ambapo moja ya kazi hizo ni unyanyuaji wa tuta la Bwawa la Mindu.

Post a Comment

0 Comments