SUAMEDIA

SUA yaonesha namna malisho bora yanavyoweza kupunguza migogoro

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Kitengo cha Malisho, kimeeleza kuwa kilimo cha malisho bora ya wanyama kinaweza kuwa suluhisho la kudumu la kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro, Ahmed Enock Amasha kutoka Kitengo hicho amesema kupitia teknolojia ya kuzalisha malisho ya kisasa katika maeneo madogo, wafugaji wanaweza kupunguza utegemezi wa kutangatanga kutafuta chakula cha mifugo.

Amasha amesema katika banda la Kitengo cha Malisho wanaonesha aina mbalimbali za malisho yenye tija ambayo wafugaji wanaweza kuyazalisha bila kuathiri shughuli nyingine za kilimo.

Amesema miongoni mwa malisho hayo ni jamii ya mikunde kama Alfa Alfa na Russian Comfrey, ambayo yana kiwango kikubwa cha protini na virutubisho vinavyosaidia ukuaji na uzalishaji wa mifugo. Pia yapo majani tembo kama Local Napier na Giant Juncao ambayo yana uwezo wa kustahimili ukame na kutoa mavuno mengi.

Aina nyingine za malisho ni nyasi kama Rhodes, Brachiaria na Cenchrus ambazo zinaweza kulimwa, kukatwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kulisha mifugo, hususan wakati wa kiangazi ambapo upatikanaji wa malisho huwa mdogo. Kwa mujibu wa Amasha, Giant Juncao inaweza kutoa mavuno ya hadi tani 180 kwa mwaka kwa hekta moja na kuwa na protini inayoweza kufikia asilimia 18, hivyo kusaidia kuongeza uzalishaji wa mifugo ya maziwa na nyama.

“Kwa kutumia malisho haya, mfugaji anaweza kulisha mifugo bila kutoka nje ya shamba lake. Hii inapunguza migogoro na wakulima kwa sababu hakuna kutangatanga. Pia, malisho haya yanaweza kulimwa kibiashara na kuuzwa kwa wafugaji wengine,” amesema Amasha.

Aidha, amewataka wafugaji kuwekeza zaidi katika kilimo cha malisho bora badala ya kuongeza idadi ya mifugo bila kuwa na uhakika wa chakula, akisisitiza kuwa ni bora kuwa na mifugo michache yenye tija kuliko kuwa na makundi makubwa yasiyo na faida.






Post a Comment

0 Comments