Dkt. Kikwete avutiwa na teknolojia za SUA, afurahishwa na wanafunzi kujifunza kilimo

 Na: Farida Mkongwe

Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane 2026, limeendelea kutembelewa na viongozi mbalimbali wanaofika kujionea tafiti, ubunifu na teknolojia za kisasa zinazolenga kuendeleza sekta ya kilimo nchini.

Agosti 7, 2026, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametembelea banda la SUA na kupokelewa na Menejimenti ya Chuo ikiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda.

Akiwa katika banda hilo, Dkt. Kikwete amepata maelezo ya jumla kutoka kwa Prof. Chibunda kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUA katika maeneo ya utafiti, ubunifu, teknolojia na utoaji wa elimu kwa wakulima, wafugaji na wadau wengine wa sekta ya kilimo.

Dkt. Kikwete ameipongeza SUA kwa kazi nzuri inayofanya katika kutoa elimu kwa wakulima pamoja na kuendeleza teknolojia zinazolenga kuongeza tija katika kilimo, mifugo na uzalishaji kwa ujumla.

Aidha, amefurahishwa na kuwepo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mafiga wanaosoma mkondo wa amali ya kilimo, ambao walipata nafasi ya kumweleza shughuli mbalimbali za kilimo wanazojifunza na kuzifanya kwa vitendo.

Kuwepo kwa wanafunzi hao katika banda la SUA kunaonesha umuhimu wa kuwajengea vijana maarifa na ujuzi wa kilimo tangu wakiwa shuleni, ili kuwaandaa kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo na kushiriki katika maendeleo ya kilimo cha kisasa nchini.




Comments

Popular posts from this blog

SUA yabuni mfumo wa AI wa kuhesabu vifaranga vya samaki

SUA yaibuka kinara taasisi za mafunzo na utafiti Nanenane 2026

Utafiti wa SUA wabaini ongezeko la visima na changamoto za maji Dodoma