Na: Ngolo Mboje
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mafiga wamesema mafunzo ya
amali yamewajengea uwezo wa kujifunza kwa vitendo, kutumia teknolojia za kisasa
na kujiandaa kujiajiri kupitia shughuli za kilimo na ufugaji wenye tija kwa
manufaa yao na jamii.
Wanafunzi hao akiwemo Maulidi Nyamoga na Husna Abdallah wameyasema hayo katika Maonesho ya Nanenane 2026, baada ya kupata fursa ya kuonesha na kueleza maarifa mbalimbali waliyopata kupitia mafunzo ya vitendo yanayotolewa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Wamesema miongoni mwa teknolojia walizojifunza ni mfumo wa
umwagiliaji kwa njia ya matone, unaosaidia kutumia maji kwa ufanisi kwa
kuyapeleka moja kwa moja kwenye mizizi ya mimea. Mfumo huo husaidia kuhifadhi
unyevunyevu wa udongo, kuimarisha ukuaji wa mimea na kuongeza uzalishaji wa
mazao.
Aidha, wanafunzi hao wamesema mafunzo hayo yamewaongezea
uelewa katika sekta ya mifugo, hususan kuhusu mbinu bora za utunzaji wa mifugo
zinazolenga kuimarisha afya, lishe na uzalishaji wake.
Wameishukuru SUA kwa kuwapatia mafunzo ya vitendo pamoja na
vifaa vya kujifunzia, wakisema elimu hiyo itawawezesha kujiajiri, kuwa wabunifu
na kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha shughuli za kilimo na ufugaji.
“Tunashukuru SUA kwa kutupatia mafunzo ya vitendo na vifaa
vya kujifunzia. Elimu hii itatusaidia kujitengenezea ajira, kuwa wabunifu na
kutumia teknolojia tulizojifunza katika kuboresha uzalishaji wa kilimo na
mifugo,” wamesema wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Somo la Afya ya Wanyama na
Uzalishaji katika Shule ya Sekondari Mafiga, Isack Mwamba, amesema mafunzo ya
amali yanawajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao,
pamoja na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya teknolojia za
kisasa katika kilimo na ufugaji.
Mwamba amesema ushirikiano kati ya Shule ya Sekondari Mafiga
na SUA ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu ya amali,
inayolenga kuwaandaa wanafunzi kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika
maendeleo ya sekta za kilimo na mifugo nchini.
Ameishukuru menejimenti ya SUA kwa kuendelea kutoa mafunzo
hayo kwa wanafunzi wa Mafiga Sekondari, akisema yamekuwa na mchango mkubwa
katika kuwapatia ujuzi wa vitendo unaowaandaa kwa maisha, kujiajiri na
kushindana katika soko la ajira.
0 Comments