Na:Farida Mkongwe
Wananchi wamehimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa
yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, hususan ugonjwa wa
kutupa mimba unaojulikana kitaalamu kama brucellosis na kifua kikuu cha
wanyama, kwa kuzingatia usalama wakati wa kuhudumia mifugo na kutumia bidhaa
zinazotokana na wanyama.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Mteknolojia wa Maabara katika Mradi wa Afya Moja, Elimu na Ushirikiano wa Sekta za Umma na Binafsi (OHEPP), Amina Abdallah, amesema mradi huo unatekelezwa kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, ukiwahusisha wataalamu wa afya ya binadamu, mifugo, elimu na sekta binafsi.
Amesema mradi huo, unaotekelezwa chini ya Ndaki ya Tiba ya Mifugo
na Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), unafadhiliwa
na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) pamoja na Shirika la
Japan la Utafiti na Maendeleo ya Tiba (AMED), kupitia programu ya Ushirikiano
wa Utafiti wa Sayansi na Teknolojia kwa Maendeleo Endelevu (SATREPS). Mradi huo
unalenga kuimarisha udhibiti wa brucellosis na kifua kikuu kinachoambukizwa
kati ya wanyama na binadamu katika Mkoa wa Morogoro.
Amesema katika Maonesho ya Nanenane wanaonesha baadhi ya vifaa vinavyotumika kukusanya sampuli kutoka maeneo ya utafiti na kuzisafirisha kwenda maabara kwa ajili ya uchunguzi. Pia wameonesha kifaa cha uhalisia pepe, yaani Virtual Reality (VR), kinachotumika kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna magonjwa hayo yanavyoambukizwa na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuyazuia.
Ameeleza kuwa ugonjwa wa brucellosis unaweza kuambukizwa kwa
kunywa maziwa ambayo hayajachemshwa vizuri au kumsaidia mnyama kujifungua bila
kuvaa vifaa vya kujikinga, kama vile glavu. Kwa upande wa wanyama, ugonjwa huo
unaweza kusababisha kutupa mimba, kupungua kwa uzalishaji wa maziwa na hasara
kwa wafugaji.
Aidha, amewashauri wafugaji kuhakikisha mifugo yao inapata chanjo kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa mifugo, kutumia vifaa vya kujikinga wanapohudumia wanyama na kuzingatia usafi wa mazingira. Wananchi pia wametakiwa kuchemsha maziwa vizuri kabla ya kuyatumia ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yanayoenezwa kupitia bidhaa za wanyama.
Ametoa rai kwa wananchi kutembelea banda la mradi huo katika
Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu kuhusu namna ya kuzuia magonjwa
yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kulinda afya ya jamii
pamoja na mifugo yao.
0 Comments