SUAMEDIA

Wakulima washauriwa kutumia teknolojia za kisasa kuongeza tija

 Na: Ngolo Mboje

Wakulima nchini wameshauriwa kutumia teknolojia za kisasa za kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuinua kipato na kuifanya sekta ya kilimo kuwa yenye tija zaidi.

Rai hiyo imetolewa na Leonard Mwankemwa, Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Sayansi za Chakula ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro.

Akizungumza na SUA Media, Mwankemwa amesema SUA imeendelea kubuni na kutengeneza teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kurahisisha shughuli za kilimo, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima.

Amesema baadhi ya teknolojia hizo ni mashine ya kuchanganyia mbolea na virutubisho vya udongo (Soil Amendment Mixer); mashine ya kupandia mpunga kwa mistari miwili (Two-Row Rice Planter), inayopanda kwa nafasi ya sentimita 25; mashine ya kusaga na kukaanga mdalasini (Cinnamon Roasting Machine); mashine za kutengeneza matuta (Ridger Machine); pamoja na mashine yenye matumizi mbalimbali ya BOPI Mobile, inayoweza kufyeka nyasi na kuchakata mazao tofauti.

Teknolojia nyingine ni mashine ya kupanda bila kulima ardhi (Zero-Till Planter), ambayo husaidia kupunguza usumbufu wa udongo, kuhifadhi unyevunyevu na kupunguza muda na gharama za maandalizi ya shamba.

Aidha, Mwankemwa amesema SUA imebuni mifumo ya kisasa ya umwagiliaji inayofaa kutumika katika bustani, vitalu vya mahindi na mashamba ya mazao mengine yanayohitaji maji ya kutosha. Mifumo hiyo husaidia kutumia maji kwa ufanisi, kuhifadhi unyevunyevu wa udongo na kuchochea ukuaji mzuri wa mazao.

Mwankemwa amewahimiza wakulima kutembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza matumizi ya teknolojia hizo, namna zinavyofanya kazi na jinsi zinavyoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji, ubora na thamani ya mazao yao.



Post a Comment

0 Comments