SUAMEDIA

SUA na COSTECH watafuta suluhisho la migogoro ya wakulima na wafugaji

Na: Asifiwe Mbembela

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akihitimisha Maonesho ya Nanenane Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, alizitaka taasisi zinazojihusisha na tafiti nchini kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Wafugaji Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Mradi huo wa miaka mitatu, unaofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), unatekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Kijiji cha Mtanana, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Kiongozi wa mradi huo, Prof. Sebastian Chenyambuga, amesema mradi unalenga kutafuta suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa malisho, ambayo ni miongoni mwa sababu zinazochangia migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Amesema watafiti wanachunguza aina mbalimbali za malisho zinazoweza kustahimili mazingira tofauti na kupatikana kwa muda mrefu katika mwaka.

Prof. Chenyambuga amesema mradi huo pia unahamasisha wafugaji kuwa na idadi ya mifugo inayoendana na uwezo wa maeneo yao ya malisho, hatua inayolenga kupunguza shinikizo kwenye ardhi na kuongeza tija katika ufugaji.

Mfugaji Clement Alophonce (55) kutoka Kijiji cha Mtanana amesema awali haikuwa rahisi kwake kufikiria kupunguza idadi ya mifugo aliyokuwa nayo, lakini baada ya kupata elimu kupitia mradi huo aliamua kubadili mfumo wake wa ufugaji.

“Niliamua kuuza ng’ombe wangu 56 wa kienyeji na kununua ng’ombe 14 wa kisasa. Hatua hiyo imenisaidia kwa sababu sasa sigombani tena na wakulima,” amesema Alophonce.

Kijiji cha Mtanana kina jumla ya wafugaji 1,320 wenye mifugo 7,829, hali inayofanya upatikanaji wa maeneo ya malisho kuwa changamoto kutokana na ufinyu wa ardhi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akieleza umuhimu wa mradi huo, Mkurugenzi wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema Tume hiyo imetoa shilingi milioni 400 kwa watafiti wa SUA baada ya kuwasilishwa kwa andiko la mradi, kwa lengo la kusaidia kupatikana kwa suluhisho la migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji wa nyama na maziwa yenye ubora na ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.

“Nimeona mabadiliko haya hayajabakia kwenye maandishi pekee, bali yameanza kuwa sehemu ya maisha ya wafugaji katika shughuli zao za kila siku,” amesema Dkt. Nungu.

Juhudi za SUA kwa kushirikiana na COSTECH zinaendelea kuunga mkono maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa na uwekezaji wa kimkakati katika kuongeza tija na ufanisi wa uzalishaji katika sekta ya mifugo.






Post a Comment

0 Comments