SUA yabuni mfumo wa AI wa kuhesabu vifaranga vya samaki
Na: Ngolo Mboje
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimebuni teknolojia
ya akili unde (AI) ijulikanayo kama Tilapia Fingerling Counter, inayowezesha
kuhesabu vifaranga vya samaki kwa kutumia simu ya mkononi kwa haraka na kwa
usahihi.
Ubunifu huo unalenga kurahisisha zoezi la kuhesabu vifaranga na kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa shughuli hiyo.
Akizungumza na SUA Media wakati wa Maonesho ya Nanenane,
Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Uzalishaji wa Viumbe wa Majini na Malisho,
Magoti Ernest, amesema mfumo huo unawasaidia wafugaji wa samaki kuhesabu
vifaranga kwa muda mfupi na kuongeza uhakika wa idadi wakati wa kufanya
biashara.
Ernest ameeleza kuwa mfumo huo huchukua takribani dakika tano kukamilisha zoezi la kuhesabu vifaranga, hivyo kuokoa muda unaoweza kutumika katika shughuli nyingine za uzalishaji.
“Teknolojia hii inapunguza muda wa kazi, inaongeza usahihi
wa hesabu na kumwezesha mfugaji kuendelea na shughuli nyingine kwa haraka,”
amesema.
Aidha, amesema mfumo huo unapunguza matumizi ya nguvu kazi
kwa kuwa unaweza kutumiwa na mtu yeyote mwenye simu ya mkononi. Pia unasaidia
kupunguza vifo vya vifaranga vinavyoweza kutokea wakati wa kuhesabiwa kwa
kutumia njia za kawaida.
Ernest amebainisha kuwa wazo la kuanzisha mfumo huo
lilitokana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafugaji katika kuhesabu
vifaranga kwa usahihi na ufanisi.
Ameongeza kuwa kwa sasa mfumo huo umefikia kiwango cha
usahihi cha takribani asilimia 88 na tayari unatumiwa na zaidi ya watu 50,
ambao wameanza kunufaika nao katika shughuli zao za ufugaji wa samaki.
“Nawashauri wafugaji na wadau wengine wa sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki kutumia teknolojia hii, kwa kuwa maendeleo ya teknolojia yanaenda kwa kasi. Ubunifu huu utasaidia kutatua changamoto zinazoweza kuzuia maendeleo ya kilimo na kurahisisha shughuli za ufugaji wa samaki,” amesema.
Aidha, amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya
Nanenane kufika katika banda la SUA ili kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hiyo
na kupata mafunzo mbalimbali kuhusu ufugaji wa samaki.
Comments
Post a Comment