SUAMEDIA

Mafunzo ya SUA yawawezesha wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao

 Na: Ngolo Mboje

Wajasiriamali wameendelea kunufaika na mafunzo yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), yanayolenga kuwajengea uwezo wa kuongeza thamani ya mazao kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na nafaka pamoja na mazao ya viungo.

Akizungumza na SUA Media, mjasiriamali kutoka Saadan Food Products, Grace Msongole, amesema mafunzo aliyoyapata yamekuwa chachu ya kujiajiri na kuboresha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na nafaka na viungo, ikiwemo tangawizi na iliki.

Amesema kupitia mafunzo hayo amejifunza mbinu za kuongeza thamani ya mazao, kuanzia hatua ya uchakataji wa mbegu hadi uzalishaji wa unga ulio tayari kutumika katika bidhaa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Msongole, ujuzi huo umemsaidia kuongeza ubora wa bidhaa zake na kuimarisha ushindani wake katika soko.

Amewahimiza wakulima na wajasiriamali wengine kufika SUA ili kupata mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za uchakataji wa nafaka na mazao ya viungo, hatua itakayowawezesha kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko na kuongeza kipato.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Uhamishaji wa Teknolojia kutoka SUA, Lucy Madalla, amesema chuo hicho kinaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuwajengea uwezo wajasiriamali kupitia mafunzo yanayolenga kukuza ubunifu, kujiajiri na kuongeza fursa za kiuchumi.

Ameongeza kuwa SUA pia huwakutanisha wajasiriamali na wataalamu mbalimbali ili kujifunza teknolojia na mbinu mpya za kilimo na uchakataji wa mazao.

Amesema hatua hiyo inachangia kuongeza tija katika uzalishaji, kuinua thamani ya mazao na kuboresha kipato cha wananchi.

Post a Comment

0 Comments