SUAMEDIA

Wanafunzi wahimizwa kuomba mapema programu mpya za SUA

 Na: Ngolo Mboje

Wanafunzi, wazazi na walezi wamehimizwa kujitokeza mapema kufanya udahili katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), hususan katika programu mpya zilizoanzishwa, ili kunufaika na mafunzo yanayolenga kuwajengea wahitimu ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira.

Akizungumza na SUA Media katika banda la udahili la chuo hicho kwenye Maonesho ya Nanenane 2026, Afisa Udahili wa SUA, Bi. Grace Kihombo, amesema chuo kimejipanga kuendelea kutoa elimu inayozingatia zaidi mafunzo kwa vitendo kupitia programu mpya zilizoanzishwa mwaka 2026.

Amesema programu hizo zinalenga kuwaandaa wanafunzi kuwa na maarifa, ujuzi na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali baada ya kuhitimu masomo yao.

Bi. Kihombo amezitaja programu hizo kuwa ni Shahada ya Kilimo na Elimu (Bachelor of Agriculture with Education), Shahada ya Nguo, Vitambaa na Mitindo ya Mavazi (Bachelor of Textiles and Fashion Studies), Shahada ya Uhandisi wa Ujenzi (Bachelor of Civil Engineering), pamoja na Shahada ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Kidijitali (Bachelor of Cybersecurity and Digital Forensics).

Amesema kuanzishwa kwa programu hizo ni sehemu ya jitihada za SUA za kupanua fursa za elimu ya juu na kukidhi mahitaji ya wataalamu katika maeneo ya teknolojia, viwanda, elimu na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Aidha, Bi. Kihombo ameeleza kuwa SUA ni miongoni mwa vyuo vinavyojikita katika utoaji wa mafunzo ya vitendo, hususan katika sekta za kilimo, mifugo na maeneo mengine ya kitaaluma. Wanafunzi hupata nafasi ya kujifunza kwa kutumia mashamba, mifugo, viwanda, maabara na miundombinu mingine ya chuo, jambo linalowawezesha kupata uzoefu wa moja kwa moja kabla ya kuhitimu.

Ameongeza kuwa udahili uko wazi kwa waombaji wote wenye sifa, huku akiwasisitiza kufuata vigezo vilivyowekwa na kukamilisha mchakato wa maombi mapema ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa udahili.

Pia, amewashauri wazazi, walezi na wanafunzi ambao bado hawajapata mwelekeo sahihi kuhusu programu zinazolingana na ufaulu wao kutembelea banda la udahili la SUA katika Maonesho ya Nanenane, ambako watapata ushauri wa kitaalamu utakaowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu uchaguzi wa programu za masomo.

Post a Comment

0 Comments