SUAMEDIA

Teknolojia ya kuzalisha malisho bila udongo yarahisisha ufugaji wenye tija

 Na: Ngolo Mboje

Wakulima na wafugaji nchini wamehimizwa kutumia teknolojia ya kuzalisha malisho ya mifugo bila kutumia udongo, ili kuongeza tija katika ufugaji na kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora na salama kwa mifugo.

Hayo yamesemwa na Afisa Mifugo Mfawidhi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Bw. William Hoza, wakati wa Maonesho ya Nanenane. Amesema teknolojia hiyo huwezesha uzalishaji wa malisho ndani ya muda mfupi wa takribani wiki moja, tofauti na kilimo cha kawaida kinachohitaji muda mrefu zaidi.

Bw. Hoza amesema mfumo huo hauna gharama kubwa za uzalishaji na husaidia kuboresha lishe ya mifugo, kwa kuwa malisho yanayozalishwa yana virutubisho muhimu, ikiwemo vitamini A, vinavyochangia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa uzito wa mifugo.

Ameeleza kuwa katika uzalishaji wa malisho hayo hakuna matumizi ya mbolea wala kemikali, hivyo mifugo ikiwemo kuku, bata na sungura hupata chakula salama .

Aidha, teknolojia hiyo ni suluhisho kwa wakulima na wafugaji wenye uhaba wa ardhi, kwa kuwa inawawezesha kuzalisha kiasi kikubwa cha malisho katika eneo dogo na ndani ya muda mfupi, hivyo kuongeza ufanisi wa shughuli za ufugaji.

Bw. Hoza amesema ili kupata malisho bora, ni muhimu kutumia mbegu zenye ubora, kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha pamoja na mwanga unaohitajika katika hatua zote za ukuaji.

Amewataka wakulima na wafugaji kutembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza kwa vitendo namna teknolojia hiyo inavyofanya kazi na faida zake katika kuongeza tija.



Post a Comment

0 Comments