SUAMEDIA

SUA yaandaa mafunzo ya biashara ya kilimo kwa wakulima Nanenane

 Na: Farida Mkongwe

Wakulima na wadau wa sekta ya kilimo wamehimizwa kushiriki mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane, ili kupata maarifa yatakayowasaidia kuendesha kilimo kama biashara na kuongeza tija.

Akizungumza na SUA Media katika Maonesho ya Nanenane, Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uchumi wa Kilimo na Biashara ya SUA, Anne Malando, amesema chuo kimeandaa mafunzo ya kila siku kwa wakulima na watu wengine wanaojihusisha na uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo.

Malando amesema siku za Agosti 1 hadi 3 zilitengwa kwa ajili ya usajili wa washiriki, huku mafunzo yakipangwa kutolewa kuanzia Agosti 4 hadi 7, 2026, katika banda la SUA.

Ameeleza kuwa mafunzo ya Agosti 4 yanahusu mnyororo wa thamani na sera, ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wa mazao kuelewa namna ya kuongeza thamani katika kila hatua ya uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa bidhaa za kilimo.

Kwa mujibu wa Malando, mafunzo ya Agosti 5 yatahusu masoko ya biashara ya kilimo, ambapo washiriki wataelimishwa kuhusu umuhimu wa kutambua soko kabla ya kuanza uzalishaji na namna ya kutafuta masoko yenye uhakika kwa mazao yao.

Amesema Agosti 6 mafunzo yataangazia uhasibu na usimamizi wa fedha katika biashara ya kilimo, ikiwemo namna ya kutumia mikopo kwa tija na kunufaika na huduma za taasisi ndogo za fedha zinazowahudumia wakulima.

Aidha, mafunzo ya Agosti 7 yatahusisha uhamasishaji wa rasilimali na namna ya kuanzisha biashara za kimataifa, ili kuwajengea washiriki uwezo wa kutafuta mitaji, kupanua biashara na kufikia masoko ya nje ya nchi.

Malando amewashauri wakulima na wadau wengine wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la SUA, kujisajili na kushiriki mafunzo hayo ili kupata maarifa yatakayowawezesha kuendesha shughuli zao za kilimo kwa ufanisi na faida zaidi.

Post a Comment

0 Comments