SUAMEDIA

Waziri Mkuu apongeza TPHPA kwa kuimarisha usalama wa chakula nchini na mauzo ya nje ya nchi

 Na: Mwandishi wetu - Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) kwa kazi nzuri ya kuhifadhi mbegu za asili na kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea na hivyo kuchangia utoshelevu wa chakula na kuongeza mapato.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru akitoa maelezo kwa waziri Mkuu wakati alipotembelea banda hilo kwenye maonesho wa wakulima Nanenane Jijini Dodoma.

Pongezi hizo amezitoa wakati alipotembelea banda TPHPA kabla ya kufungua rasmi maonesho ya wakulima Nanenane kitaifa Jijini Dodoma na kuelezwa kazi mbalimbali ambazo zinatekelezwa na mamlaka hiyo zinazoleta tija kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara ya uuzaji mazao nje ya nchi.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kusaidia kutimiza malengo ya Serikali hasa katika eneo la sekta ya kilimo ambayo inaajiri Watanzania wengi kuliko sekta nyingine yoyote, endeeeni kuchapa kazi nasi kwa upande wetu kama Serikali tutaendelea kuwaunga mkono katika kuboresha mazingira ya kazi zenu kwa kuwapatia vifaa na mahitaji mengine muhimu ili kuongeza tija” alisema Mhe. Nchemba.

Awali akitoa maelezo ya kazi za Mamlaka hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru amesema pamoja na majukumu mengi waliyonayo lakini wanasaida kuhakikisha mazao yanayozalishwa na wakulima nchini yanapimwa ubora wake na kufikia viwango vinavyohitaji kwenye masoko mbalimbali duniani na hivyo kuingizia taifa fedha za kigeni.

“Ili makampuni mbalimbali kutoka Tanzania yaweze kuuza mazao kwenye masoko mbalimbali nje ya nchi kuna vigezo ambavyo masoko hayo yanahitaji kwenye mazao hayo, hivyo sisi kama mamlaka tunasaidia kuhakikisha makampuni hayo yanapata bidhaa zenye kukidhi viwango hivyo na hivyo kuwezesha kufikia soko kulingana na mahitaji ya kila soko na bidhaa inapouzwa” alieleza Prof. Ndunguru.

Prof. Ndunguru amesema pia jukumu hilo linakwenda sambamba na kudhibiti visumbufu vya mazao ikiwemo Magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao ili wakulima waweze kulima kilimo chenya tija na kazi hiyo inafanywa kwa kutumia teknolojia za kisasa kabisa za utambuzi na udhibiti ikiwemo kipimo cha Vinasaba (DNA) ambacho kinauwezo wa kupima kinasaba cha kiumbe chochote  na kutoa majibu ndani ya dakika 20.

“Teknolojia hii ya kisasa tunaenda nayo mahali popote huko kwenye mshamba ya wakulima, tunachukua sampuli na kupima hapohapo shambani mkulima akiona na ndani ya dakika 20 tunapata majibu kuwa ni Kirusi gani, Bakteria gani au Fangasi yupi na kupendekeza kiuatilifu gani au mbinu gani sahihi inafaa kutumika kutatua changamoto iliyoonekana” alifafanua Mkurugenzi huyo Mkuu wa TPHPA Prof. Ndunguru.

Aidha amesema kuwa kazi nyingine ambayo TPHPA inafanya ni kutunza nasaba za mimea kwa maana ya Mbegu za asili zote na mpaka sasa benki hiyo ya mbegu ina aina elfu kumi (10,000) zimetuzwa  kutoka mikoa mbalimbali na za mazao aina mbalimbali zile za asili kabisa zinazotambuliwa na jamii na zingine zilikuwa zinaelekea kupotea lakini wamefanikiwa kuzitunza.

Pia Prof. Ndunguru amesema jukumu lingine muhimu la mamlaka hiyo ni kutoa mafunzo ya matumizi salama ya Viuatilifu pamoja na kuangalia ubora wa Viuatilifu vilivyopo na vile vinavyoingia nchini kwa kutumia mitambo na vifaa vya kisasa vilivyopo makao makuu ya TPHPA pale Arusha na kwenye ofisi za kanda ya mamlaka hiyo ili kusaidia wakulima kupata viuatilifu salama na kuvitumia kwa usahihi bila kuleta adhari kwao, mazao na mazingira.

“Kupitia jukumu hilo Mamlaka imeiongezea Serikali mapato katika mizigo ambayo inasafirishwa kutoka nchini kwenda nje ya nchi lakini pia kufanikiwa kufungua masoko mbalimbali ya bidhaa ambayo nchi yetu ilifungiwa kutokana na kutokidhi mahitaji ya masoko yao na sasa watanzania na makampuni yanauza mazao yetu kwa wingi kwenye masoko hayo “alifafanua Prof. Ndunguru.

Mamlaka ya Afya ya mimea na Viuatilifu Tanzania TPHPA inashiriki kwenye maonesho ya wakulima Nanenane kwenye kanda zote ikiwemo Pwani, Kanda ya kati Dodoma, Kanda ya Kaskazini jijini Arusha, Kanda ya Kusiki Mbeya na Kanda ya Magharibi Simiyu.


MATUKIO KATIKA PICHA WAZIRI MKUU ALIPOTEMBEA BANDA LA TPHPA KWENYE MAONESHO HAYO.









 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments