Wanafunzi Mafiga Waipongeza SUA kwa Elimu ya Kilimo kwa Vitendo
Na: Farida Mkongwe
Wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Mafiga iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),
wamekipongeza chuo hicho kwa kuwapatia elimu ya kilimo kwa vitendo
inayowawezesha kupata maarifa na ujuzi wa kujiajiri badala ya kusubiri ajira
baada ya kuhitimu masomo yao.
Baadhi ya wanafunzi waliotoa pongezi hizo ni Kalunde Hamisi, Stella Emmanuel, Amina Ibrahim na Mariam Abedi, ambao wote wanasoma kidato cha tatu, mkondo wa amali katika shule hiyo.
Wanafunzi hao wametoa pongezi
hizo wakati wa Maonesho ya Nanenane, wakiwa katika banda la SUA ambako
walionesha mbegu mbalimbali, mifumo ya umwagiliaji pamoja na mbinu rafiki kwa
mazingira za kudhibiti wanyama waharibifu mashambani.
Wamesema mafunzo ya vitendo yanawasaidia kuelewa kwa urahisi zaidi masomo wanayofundishwa darasani, kwa kuwa wanapata nafasi ya kutumia maarifa hayo moja kwa moja katika shughuli mbalimbali za kilimo.
Aidha, wameeleza kuwa ujuzi
wanaoupata unaweza kuwasaidia hata wanapokuwa majumbani kwa kuanzisha miradi
midogo ya kilimo, ikiwemo kilimo cha mbogamboga, na hivyo kujipatia chakula
pamoja na kipato.
Comments
Post a Comment