SUAMEDIA

SUA yaibuka kinara taasisi za mafunzo na utafiti Nanenane 2026

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la taasisi za mafunzo na utafiti na kushika nafasi ya tatu kwa jumla katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2026, ikiwa ni matokeo ya ushiriki wake katika kuonesha tafiti, teknolojia, ubunifu na huduma mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na maeneo mengine ya maendeleo.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) ambaye pia ni Mratibu wa Maonesho ya Nanenane kwa upande wa SUA, Dkt. Devotha Mosha, ameshukuru kwa ushindi huo na kusema mafanikio hayo ni motisha kwa Chuo kuendelea kujiandaa vizuri zaidi ili kufanya vyema zaidi katika maonesho yajayo.

Aidha, Dkt. Devotha ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa ushirikiano na uwezeshaji katika kufanikisha ushiriki wa Chuo kwenye maonesho hayo, pamoja na wafanyakazi wote walioshiriki katika maandalizi na utoaji wa huduma.

Pia amewashukuru wananchi na wadau mbalimbali waliotembelea mabanda ya SUA na kupata elimu, maarifa na taarifa kuhusu teknolojia na ubunifu unaozalishwa na Chuo.

Katika maonesho hayo halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliibuka mshindi wa kwanza wa jumla huku mshindi wa pili ikiwa ni halmashauri ya manispaa ya Temeke.

Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2026 yamefungwa rasmi Agosti 8, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, baada ya siku kadhaa za maonesho yaliyowakutanisha wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.





Post a Comment

0 Comments