Balozi wa Uganda nchini Tanzania Kanali Fred Mwesigye, amesema nchi yake itashirikiana kwa kina na Tanzania hususani Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kutokana na Chuo hicho kugundua Teknolojia ya Nyasi za JUNCAO ambayo itasaidia kutatua mgogoro wa wakulima na wafugaji nchini Uganda.
Ameyazungumza hayo Septemba 23, 2022 katika Kampasi ya Solomoni Mahlangu, kwenye ziara yake ya siku moja chuoni hapo ambayo imelenga kufahamu kwa kina Teknolojia hiyo kutoka SUA, akiongozwa na Mhadhiri Mwandamizi na Mtaalamu wa Teknolojia ya JUNCAO kutoka Idara ya Sayansi za Viumbe Hai, Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi ya SUA, Dkt. Elly Ligate pamoja na Mhadhiri Mwandamizi katika Idara hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara Dkt. Beda Mwang'onde.
“Nawashukuru sana viongozi wa Chuo hiki kuniita kuja kuwatembelea kuona nyasi za JUNCAO lakini baada ya kufika hapa nikaona mambo mengine yenye mchango mkubwa wa nchi hii ya Tanzania katika kukomboa nchi za Afrika maana yake nimeua ndege wawili kwa jiwe moja nimeona nyasi hizo lakini nimeona mchango huu sio tu kwa Uganda ila Afrika nzima”, alisema balozi huyo.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Teknolojia ya JUNCAO kutoka SUA, Dkt. Elly Ligate, amesema kwa sasa wamefika Uganda lakini matamanio yao ni kufika nchi nyingine za jirani ambapo teknolojia hii itahitajika, lakini nchini Tanzania hadi hivi sasa wamefanikiwa kuwafikia wakulima wapatao 54 katika Wilaya zaidi ya 10 ambazo ni Kilindi, Handeni, Bumbuli, Geita, Bukoba, Kagera, Mbarali, Dodoma, Kigamboni, Pwani, Morogoro na hata Kilosa.
“Ziara hii tunaichukulia kwa umakini wa hali ya juu sana kwasababu ni ziara ambayo inaongeza wigo wa matokeo ya teknolojia hii ambayo inaenda kuleta majibu katika sekta ya ufugaji kutokana na kuwa na changamoto ya malisho haipo tu Tanzania bali Afrika ya Mashariki kwa ujumla na kwa sababu tuna mahusiano ya kimataifa na Taasisi zingine kama vile Chuo Kikuu cha Kilimo na Mifugo kilichopo nchini China tunaamini teknolojia hii itafika mbali zaidi”, alisema Dkt. Ligate
Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuwa kulima nyasi za JUNCAO ni fursa kwa ajili ya kuwauzia wafugaji hasa zama hizi ambazo kuna mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la matumizi ya ardhi, kutokana na nyasi hizo kuwa na ustahimili wa kulimwa kwenye maeneo ya jangwa na hata majira ya kiangazi.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi za Viumbe Hai na Mkuu wa Idara hiyo Dkt. Beda Mwang'onde amesema kutokana na kuwa wanyama waliopo ni wengi na malisho ni haba, nyasi za JUNCAO zitaweza kutokomeza ufugaji wa kuhamahama ambao unapelekea familia nyingi za wafugaji kutelekezwa na hata watoto kutopata elimu.
Dkt. Beda aliongeza kuwa teknolojia hii ya JUNCAO ambayo ni majani ambayo yameboreshwa sana kwa zaidi ya miaka 20 ni jibu la matatizo ya chakula cha wanyama nchini lakini si kwa wanyama tu hata kutunza maeneo ambayo yameharibika kutokana na mabadiliko ya tabianchi hasa maeneo yaliyoathiriwa kwa mmomonyoko halikadhalika kwa kilimo cha uyoga.
0 Comments