Na: Siwema Malibiche
Wanawake wametakiwa kuwa na uangalifu
mkubwa katika malezi ya watoto ili kubaini kwa haraka matukio ya ukatili
yanayoweza kujitokeza katika familia ili kutengeneza vijana wenye weledi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Menejimenti Rasilimali Watu na Utawala Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bw. Peter Mwakiluma kwenye hafla fupi iliyoandaliwa na Chuo hicho kupitia Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Kimkoa katika halmashauri ya Mji Ifakara mkoani Morogoro.
Bw. Mwakiluma amesema wanawake wana wajibu
mkubwa wa kulinda watoto kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vya haki zitakavyosaidia
kuwajenga watoto na kuzalisha vijana watakaoleta maendeleo.
Aidha amewataka wafanyakazi wote wa SUA kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ili kuendelea kukitangaza Chuo kwa utendaji bora wa kazi unaozingatia ufanisi na weledi na kwamba Menejimenti ya Chuo itaendelea kuwawezesha wanawake wa SUA ili kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa sababu inatambua mchango wa wanawake katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Afisa Ustawi
wa Jamii Manispaa ya Morogoro Bi. Sidina Mathias ameupongeza uongozi wa SUA kwa
kuanzisha Dawati la Jinsia ambapo
amewataka viongozi wa dawati hilo kushirikiana na Manispaa ili kuboresha huduma
zinazotolewa huku akitoa wito kwa wazazi
na walezi kutojisahau katika malezi ya watoto.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake SUA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani SUA Bi. Enesa Mlay ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa kuwawezesha Wanawake wa Chuo hicho kuweza kushirikiana na wanawake wengine wa mkoa wa Morogoro huku akiwataka wazazi kutowaacha na kuwasahau watoto wa kiume katika malezi yao.
Mratibu wa Masuala ya Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Charles Lyimo amesema SUA ni miongoni mwa Taasisi iliyokuwa na mazingira bora katika kusimamia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wanawake na amewataka kutumia ipasavyo dawati la jinsia lililopo SUA ili kupata elimu na ushauri utakaosaidia kuijenga jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA Bw. Faraja Kamendu amewapongeza wanawake wote na wasichana walioshiriki katika Maadhimisho hayo huku akiwaasa kujiunga na vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi ili waweze kufaidika na maslahi yanayotokana na utetezi wa kuwepo kwa sauti ya Pamoja.
Picha zote na Nicholaus Roman
Zaidi bofya link hapo chini
https://drive.google.com/
0 Comments