SUAMEDIA

SUA kuanzisha Msitu wa Chuo wa Mafunzo ya Biashara mkoani Ruvuma

 

Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekusudia kuanzisha Msitu wa Chuo wa Mafunzo ya Biashara katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya Chuo hicho ya kusimamia na kuongeza uzalishaji wa mapato ya ndani ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.



Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Jengo Mtambuka la Mafunzo Agosti 6, 2024 mjini Morogoro katika Kmapasi ya Edward Moringe ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Rais wa Jamuhri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

                                        

“Msitu huo utakuwa na ukubwa wa hekta 10,000na tutautumia kwa ajili ya biashara ya Kaboni na uzalishaji wa mazao mengine ya misitu, hii inakwenda sambamba na kununua vifaa vya kisasa vya kuchaka magogo”, amesema  Mhe. Jaji Othman.

                                        

Mhe. Jaji Othman ameitaja mikakati mingine kuwa ni kuanzisha Kampuni ya uwekezaji wa Chuo na kwamba kampuni hiyo itasimamia vitengo vyote vya uzalishjai ambavyo sio vya kitaaluma vyenye uwezo wa kuzalisha mapato chuoni, kuimarisha Shamba la Biashara la Chuo lililopo Kampasi ya Solomon Mahlangu pamoja na vitengo vyote kikiwemo Kitengo cha Maziwa, Nguruwe, Shamba la Uzalishaji wa Chakula cha Mifugo na kuendelea kupanda Mkonge ambapo mpaka sasa hekari 200 zilishapandwa na mwaka huu zitavunwa hekari 100.

                                         

“Pia Baraza la Chuo linaendelea kutunga na kuboresha sera, kanuni na miongozo ya ndani kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Chuo katika maeneo yote ya kimkakati kwa kuzingatoa sheria, taratibu na kanuni  na maelekezo mengine yanayotolewa na Serikali ili kuhakikisha Chuo kinatekeleza majukumu yake ipasavyo”, amesema Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo SUA.

                              

Post a Comment

0 Comments