Na: Calvin Edward Gwabara – Morogoro.
Wanafunzi
wa mafunzo katika mradi wa AGRISPARK wametakiwa kuhakikisha kuwa vitabu
vinavyoandaliwa kwa ajili ya wakulima lazima viwe vinaeleweka kirahisi, Elimu yake
inatekelezeka, na vinapatikana kwa urahisi kupitia utambuzi mzuri wa walengwa
wa vitabu hivyo kwa kuzingatia kutumia
lugha rahisi, mifano inayofaa, na vielelezo ili kuongeza uelewa na matumizi ya
maarifa ya kilimo kwa wakulima.
![]() |
Mtafiti mwenza wa mradi wa AGRISPARK, Dkt. Nicholous Mwalukasa akifundisha namna ya kutambua mahitaji ya wakulima kabla ya kuwaandalia vitabu vya elimu. |
Kauli hiyo imetolewa na mtafiti mwenza wa
mradi wa AGRISPARK, Dkt. Nicholous Mwalukasa, alipokuwa akiwaelekeza wanafunzi
wa mradi juu ya uchambuzi wa hadhira na jinsi ya kujihusisha na jamii za
wakulima kabla ya kuanza kuandaa vitabu vya elimu kwa wakulima.
Dkt.
Mwalukasa aliendesha mafunzo hayo kwa njia shirikishi, akiwawezesha wanafunzi
kupata ujuzi muhimu wa kuwafikia na kuwasiliana kwa ufanisi na wakulima na
kusisitiza umuhimu wa kuelewa mahitaji ya wakulima, changamoto zao, na
upendeleo wao wa kupata taarifa ili kuboresha usambazaji wa maarifa ya kilimo
na kuwapa taarifa halisi wanazozihitaji.
Wanafunzi walifundishwa mbinu mbalimbali za
uchambuzi wa hadhira, ikiwa ni pamoja na tafiti za maoni, mahojiano, na majadiliano
ya vikundi lengwa na kuwaeleza kuwa ili taarifa za kilimo ziwe na matokeo
chanya, lazima zilingane na mahitaji mahususi ya wakulima kwa kuzingatia mambo
kama vile eneo, mbinu za kilimo, viwango vya elimu, na upatikanaji wa
teknolojia za mawasiliano.
“Kutengeneza maudhui ya elimu ya kilimo kwa
wakulima pekee hakutoshi, bali ni muhimu sana kutambua wakulima wenyewe
vizurina mahitaji yao ili huhakikisha kwamba taarifa hizo ndizo wanazozihitaji
na zitaweza kutumiwa kuboresha kilimo chao,” alisisitiza.
Mbali na maarifa ya kutambua wakulima,
Wanafunzi walifanya na mazoezi ya vitendo ili kuboresha ujuzi wao ambapo
walipewa madodoso ambayo wakulima wamejaza kwenye utafiti wa awali wa mradi huo
ili kuweza kuzitumia kuchambua na kutambua ili kujua hali halisi za wakulima
wanaotarajia kuwaandalia vitabu hivyo kabla ya kwenda kukutana nao
watakapomaliza mafunzo lengo likiwa kuwasaidia wanafunzi kupata ujasiri na
umahiri wa kukusanya taarifa muhimu moja kwa moja kutoka kwa wakulima.
"Wakulima
mbalimbali wana viwango tofauti vya upataji wa taarifa, kuanzia vyombo vya
habari vya asili kama redio na maafisa ugani, hadi majukwaa ya kidijitali kama
vile simu za mkononi na mitandao ya kijamii hivyo lazima mfikirie njia nyingi
za kusambaza maarifa ya kilimo ili kuhakikisha kuwa taarifa zinawafikia wakulima
kwa njia rahisi na inayoeleweka," alieleza.
Baada ya mafunzo, Wanafunzi walieleza
kufurahishwa kwao na mafunzo hayo na walikiri kuwa uchambuzi au kutambua
wahusika na vitabu hivyo yaani wakulima na ushirikishwaji mzuri ni sehemu muhimu za ugani
wa kilimo na mawasiliano.
PICHA ZA WASHIRIKI WAKIFUATILIA MAFUNZO HAYO
0 Comments