Na: Farida Mkongwe
Katika kuhakikisha mazingira yanaendelea kutunzwa, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii imekuja na mradi wa majaribio ya teknolojia ya Tanuri la kukausha mbao kwa nguvu za jua ambayo ni rafiki kwa mazingira kwa sababu inazuia matumizi ya nishati nyingine ambazo zinaharibu mazingira.
Mradi huo wa majaribio ambao ni
wa kwanza hapa nchini umewekwa bayana Agosti 3, 2024 na Mkufunzi Msaidizi
kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za Mazao ya Misitu, Ndaki ya Misitu,
Wanyamapori na Utalii Mbonea Mweta wakati akizungumza na SUA Media katika
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mjini Morogoro.
Akizungumzia faida za mradi huo Mkufunzi
huyo amesema utasaidia kuongeza thamani ya mbao, kupunguza gharama kwa sababu tanuri
hilo linatumia nguvu za jua ukilinganisha na matanuri mengine yanayotumia
nishati ya umeme au mafuta ya dizeli ambayo siyo rafiki kwa mazingira, pia mbao
zitaweza kudumu kwa muda mrefu na hivyo kuzuia ukataji miti wa mara kwa mara.
“Lakini tanuri hili kama
nilivyosema linasaidia kupata mbao iliyokaushwa vizuri ambayo ina vigezo vya viwango
vinavyotakiwa katika mbao na ukitumia mbao iliyokaushwa ni dhahiri kuwa utapata
samani nzuri lakini ukiunganisha mbao ambazo hazijakaushwa vizuri ni wazi kuwa
utapata changamoto ya muungo huo kuachia au mbao hizo kuharibiwa na wadudu
waharibifu na hivyo kupata hasara”, amesema Mkufunzi huyo.
Amezitaja fursa nyingine
zitakazopatikana pindi mradi huo utakapokamilika kuwa ni pamoja na kutoa ajira
kwa watumiaji wa tanuri hilo sambamba na Serikali kupata mapato kupitia
biashara ya ukaushaji mbao hapa nchini.
Amesema mradi huo utakapokamilika
na kuanza kutumika wafanyabiashara wa mbao watanufaika kwa kiasi kikubwa na
kuwataka watengenezaji wa samani kutumia mbao zilizokauka ili kuondoa
malalamiko ya wateja wao wanaolalamikia samani zao kuharibiwa na wadudu
waharibifu.
0 Comments