Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Imeelezwa kuwa Mipango sahihi na uandaaji wa
vifaa vya mafunzo ina mchango mkubwa katika kuhakikisha ujifunzaji mzuri na
uhaulishaji wa maarifa kwa wakulima.
![]() |
Prof. Athman Kyaruzi Ahmad kutoka Idara ya Ugani wa Kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akizungumza na Wanafunzi hao |
Hayo yamebainishwa na Prof. Athman Kyaruzi Ahmad kutoka Idara ya Ugani wa Kilimo katika Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati wa mafunzo ya mradi wa AGRISPARK, kwa Wanafunzi wanaopewa
mafunzo ya kuandaa vijitabu vidogo vinavyolenga kutoa majibu ya changamoto
mbalimbali na mbinu bora za kilimo kwa
wakulima nchini.
Akizungumza na wanafunzi watafiti
hao wa mradi, Prof. Kyaruzi alisisitiza
kuwa malengo yaliyoainishwa vyema husaidia katika kupanga maudhui
yanayohitajika, yenye manufaa, na rahisi kueleweka kwa wakulima ili waweze
kuyatumia kuboresha shughuli zao za kilimo.
“Ni muhimu kutambua walengwa wa vitabu hivyo kabla
ya kuandaa nyenzo za mafunzo iwe ni wakulima wadogo, maafisa ugani, au
wanafunzi wa kilimo ili kuhakikisha kuwa maudhui yanawiana na mahitaji yao,
kiwango chao cha elimu, na maarifa waliyonayo," alifafanua Prof. Kyaruzi.
Kwa mujibu wa Prof. Ahmad, uchaguzi wa aina sahihi ya vifaa vya mafunzo ni muhimu kwa
ujifunzaji wenye tija kwa kwakuwashauri Wanafunzi hao kufikiria kwa kina kuhusu
muundo unaofaa kwa wakulima, ikiwa ni vijitabu
vyenye picha, mwongozo wa hatua kwa hatua, au nyenzo za rejea na
kusisitiza kuwa lugha iwe nyepesi na
inayoeleweka na iwe na mifano halisi ili wakulima waweze kuelewa na
kutumia maarifa hayo kuboresha kilimo chao.
Akizungumzia umuhimu wa kuweka malengo bayana ya mafunzo
katika maandalizi ya vifaa vya elimu amesem kuwa malengo haya yanapaswa kuwa yanayopimika na yanayoweza kufikiwa,
yakilenga kuongeza ujuzi wa wakulima, kuboresha mbinu zao, na kuhimiza mabadiliko
chanya katika kilimo.
Kuhusu mpangilio na uwasilishaji wa maudhui, Prof. Ahmad aliwataka Wanafunzi watafiti kuhakikisha kuwa taarifa
zinafuata mtiririko mzuri, huku dhana ngumu zikivunjwa katika sehemu rahisi
kueleweka na kuwataka kutumia michoro,
vielelezo, na mifano halisi ili kusaidia wakulima, hasa wale wenye ujuzi
mdogo wa kusoma na kuandika, kuelewa vyema.
Pia mbobevu huyo kwenye masuala
ya Kilimo na Ugani kutoka SUA alisisitiza umuhimu wa kufanyia majaribio vifaa hivyo kabla ya kusambazwa kwa wingi.
"Kabla ya kusambaza vijitabu
hivi kwa kiwango kikubwa, ni muhimu kuvijaribu kwa kundi dogo la wakulima ili
kutathmini ufanisi wake kwani maoni yao yatasaidia kuboresha maudhui ili yawe
ya vitendo na yanayokidhi mahitaji yao," alisema Prof. Kyaruzi.
Mradi wa AGRISPARK, unaosimamiwa
na SUA, unalenga kuziba pengo la maarifa ya kilimo kwa kuwawezesha wanafunzi
watafiti kuandaa nyenzo za elimu kwa wakulima na kupitia mpango huu, wakulima wadogo kote
Tanzania wanatarajiwa kupata taarifa zilizopangiliwa vizuri na zenye msingi wa
tafiti ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto kuu za kilimo
PICHA WASHIRIKI WAKIFUATILIA MAFUNZO HAYO
0 Comments