SUAMEDIA

Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SNAL) imewataka wafugaji wa Kuku kusoma na kufuatilia Vitabu na Majarida kwa lengo la kujifunza njia bora

 Na Hadija Zahoro

Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SNAL) iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imewataka wafugaji wa kuku nchini kusoma na kufuatilia majarida pamoja na vitabu vinavyopatikana katika maktaba hiyo kwa lengo la kujifunza njia bora za utotoleshaji wa vifaranga. 

Picha Maktaba


Akizungumza na SUA Media, Afisa Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo, Kitengo cha Marejeleo na Taarifa kwa Jamii, Bi. Editha Njau amesema wafugaji wanatakiwa kuwa na tabia ya kujisomea kwa sababu wanaamini kuwa kila kaya inafuga hivyo jukumu lao ni kutoa elimu ili waweze kufuga kwa tija na kujikwamua kiuchumi pamoja na kuepuka hasara zitokanazo na kutozingatia njia bora za ufugaji.

Bi. Editha amewaomba wafugaji kuzingatia njia bora za kutotolesha vifaranga kuanzia misingi yake ikiwemo jogoo mwenye afya nzuri pamoja na mtetea mwenye umbo kubwa kwani ni lazima kuwepo na uwiano wa umbo kati ya jogoo na mtamia.

“Kwanza kabisa unatakiwa kufahamu sifa za jogoo mwenyewe atakayekwenda kumpanda yule mtetea, siyo jogoo aliye dumaa  lakini kwa upande wa mtetea lazima awe na umbo kubwa pamoja na uwezo wa kutotoa mayai mengi na madini yote hayo yapo katika maktaba zetu, hivyo tunatoa elimu mara kwa mara lakini leo tumeamua kuwadokezea”,  anaeleza Bi. Editha.  

Ameeleza kuwa licha ya kuwepo na vitabu pia mfugaji anaweza kujisomea kwa njia ya simu Janja popote pale alipo na kupata mafunzo mbalimbali kwani waandaaji wa vitabu hivyo ni wataalamu waliobobea katika sekta ya ufugaji pamoja na sekta nyingine zinazohusiana na kilimo.

Aidha, Bi. Editha amewaomba wadau kutoa maoni yao kwa kile ambacho watahitaji kukifahamu zaidi hasa kuhusu suala la utotoleshaji wa vifaranga kupitia SUA Media ili waweze kuongeza ujuzi wa njia tofauti za kupata mazao  yaliyo bora.

Amesema kuku bora hutaga mayai ya kutosha, awe na uwezo wa kulalia mayai yake na kutotoa huku mfugaji naye akiwa anazingatia uhifadhi Mzuri wa mayai hayo.

Nae Grayson Kivunge kutoka Kitengo cha Wasomaji amesema mwitikio wa wadau katika suala la kusoma vitabu katika Maktaba hiyo hasa katika Kitengo cha  Huduma ya Usomaji ni mzuri na kwamba wanaendelea kuwakaribisha sana wafugaji waweze kujifunza kupitia Maktaba hiyo.


Picha Maktaba



Post a Comment

0 Comments