NA; AYOUB MWIGUNE
Wataalamu wa Kilimo nchini wametakiwa kutumia taaluma waliyonayo
kuhamasisha wakulima kutumia Mbegu zilizo thibitishwa na Mamlaka ya Kuthibiti
Ubora wa Mbegu (TOSCI) ili kuondokana na changamoto ya wakulima walio wengi kutumia
Mbegu zisizo na ubora na kupelekea kupata Mazao machache yasiyo na tija na
wengi wao kushindwa kuendelea na shughuli za Kilimo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe jijini Dodoma katika
mkutano wa mwaka wa Umoja wa Wanasayansi wa Mazao na Vipando Tanzania (CROSAT)
ambapo ameitaka Jumuiya hiyo kujadili namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa
mbegu na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Prof. Shemdoe amesema makusanyo mengi ya Mapato yanayotegemewa na Serikali
za mitaa yanategemea Kilimo hivyo kutakapokuwa na Mazao na Mbegu bora Serikali
za mitaa zitaweza kupata mapato kwa wingi lakini pia kutakuwa na maendeleo
katika kaya.
Vile vile Prof. Shemdoe amesema Tanzania inategemea Chakula ambacho
kinatokana na Kilimo hivyo Mkutano wa mwaka wa Umoja huo wa Wanasayansi wa
Mazao na Vipando Tanzania unabeba majibu ya maswali mengi ambayo Wakulima wanatamani
kuyapata kutoka kwa Wataalam hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Patrick Ngwediah amewashauri CROSAT kutoa elimu kwa Wakulima
juu ya matumizi sahihi ya Mbegu.
Naye Mwenyekiti wa sasa wa CROSAT Prof. Kallunde Sibuga ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
amesema umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwakusanya pamoja Wanasayansi wa
Mimea.
Aidha akielezea kuhusu dhumuni la kukutana Prof. Sibuga amesema lengo hasa
ni kupanga Mikakati kuhusu kuboresha Katiba yao ili kuongeza tija katika kilimo
cha mazao, kubadilishana mawazo na kuishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusu Mazao.
Katika Video
0 Comments