SUAMEDIA

Wanafunzi wa SUA Waaswa Kutumia Vyema Taarifa Huria Mitandaoni

 Na: Jabir Jabil - Morogoro

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamehimizwa kuchangamkia fursa ya taarifa huria (Open Data) zinazopatikana mitandaoni kwa manufaa yao katika masomo na kujiwekea mazingira bora ya ajira wakiwa chuoni na baada ya kuhitimu.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia na Habari wa SUA, Prof. Camilius Sanga, wakati akihitimisha maonesho ya siku mbili yaliyoandaliwa na Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Sokoine (SNAL)


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia na Habari wa SUA, Prof. Camilius Sanga, wakati akihitimisha maonesho ya siku mbili yaliyoandaliwa na Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Sokoine (SNAL). Maonesho hayo yaliyojikita katika kauli mbiu "Taarifa Huria ili Kukabiliana na Changamoto Nyingi" (Open Data to Tackle the Poly-crisis) yalizingatia dhima ya "Taarifa Huria kwa Usalama wa Chakula" (Open Data for Food Security), kama ilivyochaguliwa na SNAL.

Prof. Sanga alieleza kuwa ingawa taarifa huria zina faida lukuki, pia zina changamoto, hivyo watumiaji wanapaswa kuwa makini na kuchanganua taarifa hizo kwa uangalifu. Alisisitiza kuwa, kwa kuzingatia ongezeko la matumizi ya simu janja na mitandao ya kijamii, wanafunzi wanaweza kutumia taarifa hizo si tu kwa ajili ya masomo, bali pia kwa kujiongezea kipato. Alitoa mfano wa jinsi mwanafunzi anavyoweza kuanzisha jukwaa la mijadala au kutoa maarifa mtandaoni kwa kutumia vyanzo vya taarifa huria, na hivyo kupata wafuatiliaji wengi—fursa inayoweza kuwavutia wadhamini au makampuni kuweka matangazo na kumletea mapato.

Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa jamii kujifunza, kushirikiana, na kuelewa namna bora ya kutumia taarifa huria kwa maendeleo yao. SNAL, kupitia maonesho hayo, ilionesha upatikanaji wa machapisho mbalimbali ya kielectroniki (e-resources) yanayowahusu wanafunzi, wahadhiri, na jamii kwa ujumla. Maonesho hayo yalifanyika katika viwanja vya SNAL, Kampasi ya Edward Moringe Sokoine, Morogoro.

PICHA ZA WASHIRIKI WAKIFUATILIA NASAHA ZA UFUNGAJI MAONESHO.










Post a Comment

0 Comments