SUAMEDIA

Wanawake nchini wametakiwa kuwekeza na kuchangamkia fursa za maendeleo

 

Na: Siwema Malibiche

Wanawake nchini wametakiwa kuwekeza  na kuchangamkia  fursa ipasavyo huku wakiwajibika katika maeneo yao ya kazi ili kujikwamua kiuchumi kwa maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa  na Prof. Yasinta Muzanila wakati akifungua Semina ya siku moja kwa wafanyakazi wanawake  na wasichana wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  mkoani Morogoro iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu  “Elimu ya  mikopo nafuu na uwekezaji kwa wanawake”.

Aidha Prof. Muzanila amesema kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuleta usawa wa kijinsia kwa kuzingatia haki na usawa huku ikijulikana kuwa wanawake wana msukumo mkubwa katika jamii ambao kama ukitumika ipasavyo itakuwa chachu kwa maendeleo ya Tanzania hasa kwa  kutambua mchango wa wanawake na wasichana wote ambao wanajishughulisha na ujasiriamali.

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa mitaji kwa wanawake vijana na watu wenye ulemavu inayosaidia kuendeleza uwekezaji katika sekta mbalimbali unaosaidia kujikwamua kiuchumi”, amesema Prof. Muzanila.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Menejimenti Rasilimali Watu na Utawala SUA Bw. Peter Mwakiluma amesema Menejimenti inatambua mchango wa wanawake na wasichana katika Taasisi na ndiyo sababu imekuwa ikiwapa nafasi mbalimbali za uongozi na amewataa kuendelea kuonesha uwezo wao na kujiendeleza kitaaluma.

Naye  Mshauri wa Masuala ya Uwekezaji  CPA Asegelisye Lupogo  ambaye ni mtoa mada katika semina hiyo amesema elimu ya fedha imekuwa tatizo kwa watu wengi  ambalo linapelekea  biashara za watu wengi kushindwa kuendelea hivyo amewataka washiriki wote wa mafunzo hayo  kuyafanyia kazi yale yote ambayo wamejifunza ili kupata faida kiuchumi.


Akizungumza kwenye semina hiyo, Mjumbe wa Dawati la Jinsia SUA Dkt. Emma Njau amesema katika kuadhimisha miaka 30 ya Azimio la Beijing, Tanzania imepiga hatua kwani ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali umeongezeka ikiwemo kushika nafasi za uongozi, ushiriki katika masuala ya afya na ustawi kwa wanawake na uwekezaji wa kiuchumi huku akisema  ni vyema kusimamia haki na usawa katika jamii kwa kuendelea kuboresha ushirikiano katika sekta zote.

Semina ya Wafanyakazi wanawake  na wasichana wa SUA imefanyika ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambacho kilele chake ni Machi 8 kila mwaka ambapo kwa mwaka 2025 maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” na kwa mkoa wa Morogoro yatafanyika katika mji wa Ifakara.







Picha zaidi bofya hapo chini

https://drive.google.com/drive/folders/1pE9pGUw5Da4l2h0dUoUzt1OrczFA0S9A?usp=sharing



Post a Comment

0 Comments