Na: Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeuomba Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma,
(PSSSF) kutangaza huduma za kilimo zinazotolewa na Chuo hicho kwa wafanyakazi
pindi wanapotoa elimu kuhusu Mafao ya kustaafu ili wafanyakazi hao waweze
kunufaika na fursa mbalimbali za kilimo ikiwemo mafunzo yanayotolewa na SUA.
Ombi hilo
limetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa
Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala, akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Prof.
Raphael Chibunda wakati akifungua Semina muhimu kwa wafanyakazi wa SUA
kuhusiana na uelewa juu ya mabadiliko ya Kikotoo kwa wastaafu ambayo
imefanyika SUA mjini Morogoro.
‘‘Chuo chetu
ni Chuo Kikuu cha Kilimo na kina fani nyingine kwa hiyo sio mbaya kule
mnapoenda kutoa elimu kwa hao wanaokaribia kustaafu mkawaambie kuwa wakikipata
hicho kikokotoo basi wawekeze katika fursa mbalimbali za Kilimo na kilimo cha
bustani, utengenezaji wa thamani na kadhalika’’, amesema Prof. Mwatawala.
Kwa upande
wake Meneja wa Matekelezo kutoka PSSSF anayeshughulikia Uandikishwaji wa
Wanachama pamoja na Michango Bw. Victor Kikoti amesema faida kubwa zaidi
kuhusiana na Kikokotoo kipya kwa wastaafu ni kuwa na Mfuko endelevu ambapo
kupitia kikokotoo hicho mfuko utaweza kulipa wastaafu wa sasa, wastaafu wa kesho ambao kwasasa bado ni vijana na wanaajiriwa.
Amesema
kupitia kikokotoo kutakuwa na Pensheni ambayo itatazama moja kwa moja hali ya
Uchumi na kuwapandishia pensheni kila baada ya miaka mitatu wastaafu wote
waliojiandikisha ambapo pia mfuko utatoa dhamana ya pensheni kwa wategemezi
wake kisheria pindi mstaafu anapofariki.
‘‘Pensheni hii inayoenda kulipwa na Kikokotoo imetathminiwa kuzingatia michango aliyochanga mstaafu, kipindi alichochanga na hali ya maisha ya nchi yetu na kama nilivyoeleza kwenye semina walikuwepo Vyama vya Wafanyakazi na Wawakilishi wa Waajiri ambao katika tathimini yao wameangalia hali ya uchumi, hali ya maisha na uendelevu wa mfuko hivyo niwatoe hofu kwani Wataalam kwa kushirikiana TUCTA wametazama hali ya maisha na wakazingatia kwamba tutaweza kuishi na mfuko utaweza kutulipa leo, kesho na hata baadae’’, amesema Victor Kikoti.
Mmoja wa washiriki katika Semina hiyo Bw. Stephano Kingazi ambaye ni Mtumishi kutoka SUA amesema semina hiyo imekuwa ni ya manufaa zaidi kwao kwani imewapatia uelewa juu ya Kikokotoo ikiwemo kanuni iliyotumika juu ya kutafuta mkupuo ambao wengi walikuwa wanajiuliza maswali mengi hivyo imefafanuliwa vizuri na kutoa majibu jambo muhimu ni kuendelea kuelimishana.
Naye Prof. Yasinta Muzanila amesema kuwa yeye kama mstaafu mtarajiwa na mshiriki katika semina hiyo amepata uelewa wa kutosha juu ya Kikokotoo kwani kuambiwa kitu na muhusika kimempatia taarifa sahihi na za uhakika na kumtoa wasiwasi.
Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa na Chama cha Wafanyakazi RAAWU Tawi la SUA kwa lengo la kuwawezesha Wafanyakazi wa Chuo hicho kupata elimu juu ya mabadiliko ya kikokotoo kinachotumika kwa wastaafu.
KATIKA VIDEO BOFYA HAPA CHINI
0 Comments