Na: Hadija Zahoro
Chuo Kikuu cha So
koine cha Kilimo SUA kimeanzisha matengenezo ya tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji wa mashamba yenye ekari takribani 50 yaliyopo chuoni hapo.
Zoezi hilo la matengenezo ya tanki hilo limewashirikisha Wanafunzi wa mwaka wa pili katika Kozi ya Uhandisi wa Ndani na wengine kutoka vyuo vingine nchini kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo ili kujiongezea ufanisi wa kile wanachojifunza darasani.
Akizungumza na SUA Media Mhandisi Jackson Masakia wa Idara ya Uhandisi (Menejimenti ya Uhandisi wa Rasilimali Maji) ambaye ndiye Msimamizi wa Ubora wa zoezi hilo pamoja na kusimamia wanafunzi hao katika masomo yao kwa vitendo, amesema wapo katika hatua ya mwisho wa zoezi hilo ambapo chuo kimetoa vifaa mbalimbali ili kukamilisha zoezi hilo.Amesema kwa kushirikiana na walimu pamoja na wataalamu mbalimbali,wanafunzi hao wa mwaka wa pili wameweza kuunda kuanzia msingi wa shughuli nzima za ujenzi, safu pamoja na kufahamu ubora wa zege kupitia kupima katika Maabara mpya zilizopo chuoni hapo.
‘‘Ishu kubwa tunayoifanya hapa ni kutengeneza uelewa kwa wanafunzi juu ya kazi za umwagiliaji pamoja na kazi za ufundi, na hapa unapoona wanafunzi wameweza kudizaini kwa kushirikiana na walimu wao kuanzia kwenye base mpaka kolamu’’, ameeleza Mhandisi Masakia
Ameeleza kuwaanafurahi kuona Chuo kimebadilisha mwelekeo ukilinganisha na zamani kwani wameweka msisitizo kwa wanafunzi wa mwaka wa pili kubaki chuoni ili kujifunza masomo yao kwa vitendo wakiwa chuoni ili kuwafanya wawe bora baada ya kumaliza masomo yao kwa upande wa umwagiliaji na ufundi.
Kwa upande wake Elizabeth Michael Elkana Mwanafunzi chuoni hapo katika Kozi ya Uhandisi wa Kilimo pamoja na Mipango ya Ardhi, amesema amejifunza zaidi njia sahihi za kuchanganya zege ili aweze kupata mchanganyiko sahihi pamoja na masuala mengine ya mashambani ikiwemo kuandaa mashamba hivyo, amewaomba wanafunzi wasichukulie SUA ni chuo kigumu badala yake waje kujifunza.
Nae, Philipo Leonard Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika kozi ya Uhandisi wa Umwagiliaji na Rasilimali Maji amesema katika mafunzo hayo kwa vitendo amejifunza kuwa ataweza kukuza mazao hata katika kipindi cha kiangazi pamoja na kufahamu vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kuandaa shughuli za ujenzi na kwamba baada ya kuhitimu masomo yao watakuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe
0 Comments