SUAMEDIA

Uzinduzi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET)

Serikali ya Tanzania imeahidi kuwasomesha nje ya nchi Wahadhiri wa Vyuo Vikuu kikiwepo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  kwa lengo la kusaidia Wahadhiri hao kutoa Elimu yenye ubora na kukabiliana na Soko la Ajira kimataifa.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa HEET.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 13, 2022 na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa uzinduzi  wa Mradi wa HEET wenye lengo la kuboresha Elimu nchini kwa kuwapeleka Wahadhiri kusoma nchi mbalimbali ambapo inategemewa mradi huo kunufaisha Vyuo 14 nchini.

 “Mradi huu ni mkubwa na wa pekee kabisa kwani unatoa hamasa kuisukuma Tanzania katika suala zima la Elimu pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Vyuo ikiwa ni pamoja na mitaala ya kufundishia na kujifunzia” alisema Prof. Mkenda.

 Aidha akitoa maagizo kwa wasimamizi wa Mradi wa HEET Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis  Michael amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa mradi huo pamoja na fedha ili zitumike kulingana na malengo yaliyokusudiwa na kusema kuwa  ikibainika kuna ujanja unafanyika ili kuharibu utekelezaji wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria.

 Naye Msimamizi wa Mradi wa HEET kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Winfred Mbungu amesema  SUA itanufaika katika maeneo saba ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo ya zamani, udhamini wa masomo kwa wafanyakazi kwa kozi za muda mrefu na muda mfupi,kuongeza uwezo wa SUA kwa upande wa mapato ya ndani vilevile mradi utasaidia kunufaaisha watu wenye mahitaji maalum.

Mradi wa HEET ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano 2021-2026 umezinduliwa jijini Dar es Salaam ukihusisha uwepo wa Benki ya Dunia, Wizara ya Fedha, Makamu Wakuu wa Vyuo (Taasisi za Elimu ya Juu na Afya), Waratibu wa Mradi kutoka Taasisi zinazonufaika pamoja na Wawakilishi wa waliopata ufadhili.




 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael akitoa maagizo kwa wasimamizi wa Mradi wa HEET wakati wa Uzinduzi.






Post a Comment

0 Comments