SUAMEDIA

Wanawake wachangia mafanikio ya miaka 50 ya Ndaki ya Tiba ya mifugo SUA

 Na: Farida Mkongwe

Wanawake waliosomea na kufanya kazi katika Ndaki ya Tiba ya Mifugo na Sayansi za Afya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu, utafiti na ufundishaji, licha ya changamoto na mitazamo iliyokuwepo hapo awali kwamba taaluma ya tiba ya mifugo inafaa zaidi kwa wanaume.

Akizungumza katika mahojiano maalumu kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Ndaki hiyo, Dkt. Faraja Hosea Mpagike amesema wanawake wamekuwa chachu ya maendeleo ya taaluma hiyo kupitia ufundishaji, tafiti na kuimarisha ubora wa wataalamu wanaohitimu, hatua inayochangia maendeleo ya sekta ya mifugo na taifa kwa ujumla.

Akielezea safari yake ya kitaaluma, amesema alipokuwa akisomea shahada ya kwanza ya tiba ya mifugo alikumbana na kauli za kumkatisha tamaa kutokana na kuwa mwanamke, lakini hakukubali changamoto hizo zimrudishe nyuma, badala yake aliendelea kujituma hadi alipofanikiwa kuhitimu masomo ya miaka mitano na baadaye kuajiriwa kama Mkufunzi Msaidizi wa Awali (Tutorial Assistant).

Amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, wanawake katika taaluma hiyo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan kusawazisha majukumu ya kazi na maendeleo ya kitaaluma, jambo linalohitaji nidhamu katika matumizi ya muda, ubunifu na juhudi binafsi ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Dkt. Faraja ameeleza kuwa mafanikio ya wanawake waliotangulia katika taaluma ya tiba ya mifugo yamekuwa kichocheo kwa wasichana na wanawake wengine kujiunga na fani hiyo, kwani kuwepo kwa wanawake waliofanikiwa katika elimu, utafiti na ufundishaji kunawajengea ujasiri wa kuamini kuwa wanaweza kufikia mafanikio sawa na wanaume.

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 50, amesema anajivunia kuwa sehemu ya historia ya Ndaki hiyo ambayo imefanikiwa kuzalisha wataalamu wanaohudumu katika sekta mbalimbali nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha tafiti na matumizi ya teknolojia ili kuongeza ubora wa elimu na kukidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, amewahimiza wasichana wanaotamani kujiunga na taaluma ya tiba ya mifugo kuamini uwezo wao, kusoma kwa bidii na kuzichukulia changamoto kama fursa za kujifunza na kukua kitaaluma, huku akitoa wito kwa wadau wa Ndaki hiyo kuendeleza mshikamano na mafanikio yaliyopatikana katika miaka 50 ili kuzalisha wataalamu watakaoendelea kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa.

Post a Comment

0 Comments