Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshauriwa kuendelea
kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kufundishia tiba ya mifugo, ikiwemo
vifaa vya mafunzo vinavyoiga mazingira halisi (Simulation), ili kuwawezesha
wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo bila kutegemea matumizi ya wanyama hai katika
kila hatua ya mafunzo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Ndaki ya Tiba ya Mifugo na Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mhadhiri wa Idara ya Upasuaji na Uzazi wa Wanyama, Dkt. Doreen Ndossi, amesema matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kuongeza ufanisi wa mafunzo, hususan wakati huu ambapo idadi ya wanafunzi wanaojiunga na taaluma ya tiba ya mifugo inaendelea kuongezeka.
Amesema vifaa hivyo vitawezesha wanafunzi kujifunza na kurudia
taratibu mbalimbali za kitabibu, ikiwemo kutoa damu na kufanya upasuaji, kabla
ya kufanya mafunzo kwa wanyama halisi, hatua itakayosaidia kuimarisha ujuzi wao
huku ikipunguza matumizi ya wanyama hai katika hatua za awali za kujifunza.
Dkt. Ndossi ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 50, Ndaki
hiyo imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, vifaa vya tiba,
utafiti na mafunzo kwa vitendo, ambapo mabadiliko hayo yamechangia kuongeza
uwezo wa taasisi katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika
sekta ya mifugo.
Akizungumzia ushiriki wa wanawake katika taaluma hiyo, amesema
kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wa kike, akieleza kuwa wakati baadhi ya
wanawake waliotangulia walikuwa wakisoma katika madarasa yenye idadi ndogo sana
ya wanawake, hivi sasa yeye anafundisha darasa lenye wanafunzi wa kike zaidi ya
30, jambo linaloonesha hatua zilizopigwa katika kuwavutia wanawake kusomea tiba
ya mifugo.
Amesema licha ya changamoto na mitazamo iliyokuwepo hapo awali
kwamba taaluma ya tiba ya mifugo ni ngumu na inafaa zaidi kwa wanaume, wanawake
wameendelea kuthibitisha uwezo wao kupitia elimu, utafiti na ufundishaji, huku
akisisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi kuanzia
ngazi za shule za msingi na sekondari.
Aidha, Dkt. Ndossi amesema maadhimisho ya miaka 50 ni fursa ya
kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuweka misingi ya maendeleo ya baadaye,
ikiwa ni pamoja na kuongeza madarasa ya kisasa, vifaa vya kufundishia na
mazingira bora ya kujifunzia, ili Ndaki hiyo iendelee kutoa wataalamu wenye
uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika miaka 50
ijayo.

0 Comments