Na: Ayoub Mwigune
Mashindano ya Shirikisho la
Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA)
yametajwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha afya za watumishi, kukuza nidhamu na
kujenga maadili mema kupitia ushiriki wa michezo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliyemwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amesema michezo ina mchango mkubwa katika kujenga afya bora ya mwili na akili, kuimarisha mshikamano na kukuza mahusiano mema baina ya watumishi katika taasisi mbalimbali.
Amesema ushiriki wa watumishi
katika michezo huwasaidia kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kuimarisha afya
zao na kuongeza ari ya kutekeleza majukumu ya kila siku katika maeneo yao ya
kazi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya michezo, ikiwemo nidhamu, kuheshimiana, uaminifu, uvumilivu na ushindani wa haki, akiwataka washiriki kutambua kuwa lengo la mashindano si kupata ushindi pekee bali pia kujenga umoja na mahusiano mema.
Ameeleza kuwa SHIMMUTA ina
historia ya muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1967 na imeendelea kuwa
jukwaa la kuwaunganisha watumishi kutoka mashirika ya umma, taasisi na
makampuni binafsi kupitia michezo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa, amewataka watumishi wa chuo hicho wanaoshiriki mashindano ya SHIMMUTA kuzingatia nidhamu na maadili ya michezo pamoja na maadili ya kazi.
Prof. Muhairwa amesisitiza kuwa
watumishi wanapaswa kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia kanuni na taratibu
za michezo, kuheshimu washindani wao na kudumisha mshikamano, akieleza kuwa
nidhamu inayojengwa kupitia michezo inapaswa pia kuonekana katika utekelezaji
wa majukumu yao ya kila siku kazini.






0 Comments