Na: Farida Mkongwe
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhusu ubora wa maji ya chini ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma umebaini uwepo wa viwango vya juu vya chumvi, madini na kemikali katika baadhi ya vyanzo vya maji, huku ukionesha umuhimu wa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira ili kuboresha ubora wa maji na kulinda afya za watumiaji
Matokeo hayo yamewasilishwa jijini Dodoma katika Warsha ya Wadau wa Mradi wa CLARITY kupitia Maabara ya Mabadiliko (Transformation Lab), ambapo watafiti na wadau mbalimbali wamejadili changamoto za ubora wa maji na mbinu za kuyatibu ili kuhakikisha yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu na shughuli za kilimo.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mtafiti wa mradi kutoka SUA, Poliect Ngowi, amesema utafiti uliofanyika katika maeneo ya Dodoma Mjini, Bahi, Chemba na Chamwino umeonesha kuwa baadhi ya vyanzo vya maji ya chini ya ardhi vina viwango vya juu vya madini na kemikali, ikiwemo nitrati, kloridi, kalsiamu na magnesiamu, hali inayoweza kuathiri ubora wa maji na matumizi yake.
Ngowi amesema uchambuzi wa sampuli za maji umeonesha kuwa asilimia 47.8 ya sampuli zilizochunguzwa zilikuwa na viwango vya nitrati vilivyozidi ukomo uliotumika katika tathmini, huku asilimia 53.7 zikiwa na viwango vya juu vya kloridi. Aidha, tathmini ya ubora wa maji imeonesha kuwa maeneo ya Bahi na Dodoma Mjini yalikuwa na madaraja ya ubora wa kuanzia mzuri hadi bora sana, wakati Chemba na Chamwino yalikuwa na madaraja ya ubora hafifu hadi mzuri kwa matumizi ya kunywa.
Ameeleza kuwa katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo, watafiti wamechunguza matumizi ya malighafi zinazopatikana katika mazingira asilia, ikiwemo mkaa unaotokana na mifupa ya wanyama kwa kuchanganywa na nyenzo nyingine, ambapo matokeo yameonesha uwezo wa kupunguza baadhi ya metali kama risasi na zinki. Hata hivyo, amesema mbinu hizo zina mipaka katika kuondoa chumvi na ugumu wa maji, hivyo kuna umuhimu wa kutumia mifumo mseto ya utibuaji kulingana na aina ya uchafuzi uliopo.
Aidha, Ngowi amesema utafiti umebaini kuwa shughuli za kibinadamu, zikiwemo matumizi ya vyoo vya shimo, mifumo ya majitaka na kemikali za majumbani, pamoja na hali ya kijiolojia ya maeneo husika, zinaweza kuchangia uchafuzi wa maji ya chini ya ardhi. Ameongeza kuwa licha ya maji mengi yaliyofanyiwa tathmini kuonekana kuwa na uwezekano wa kutumika katika umwagiliaji, baadhi ya sampuli zimeonesha viwango vya chumvi vinavyoweza kuathiri uzalishaji wa mazao.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa mara kwa mara wa ubora wa maji, kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira za utibuaji wa maji. Amesema matokeo ya utafiti huo yatasaidia mamlaka za maji, wataalamu na wadau wengine kupanga mikakati ya kulinda vyanzo vya maji ya chini ya ardhi, kudhibiti uchafuzi na kuhakikisha wananchi wanapata maji yenye ubora unaokidhi matumizi yaliyokusudiwa.
0 Comments