SUAMEDIA

Utafiti wa SUA wabaini hatari ya uhaba wa maji bonde la Bubu ifikapo 2030


Na: Farida Mkongwe

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Bonde la Mto Bubu mkoani Dodoma umeonesha uwezekano wa kutokea upungufu wa maji wa takribani mita za ujazo milioni 341 ifikapo mwaka 2030, kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji kwa shughuli za kilimo, ufugaji na matumizi ya majumbani.
Matokeo hayo yamewasilishwa katika warsha ya wadau wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) kupitia Maabara Shirikishi ya Mabadiliko (Transformation), iliyofanyika jijini Dodoma, kwa lengo la kujadili matokeo ya tafiti na kubainisha mikakati ya kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Uhandisi na Usimamizi wa Umwagiliaji kutoka SUA, January Job Mlomo, amesema mahitaji ya maji katika Bonde la Mto Bubu yanaendelea kuongezeka, huku upatikanaji wake ukibadilika kulingana na misimu ya mvua na kiangazi. Kwa mujibu wa utafiti huo, mahitaji ya maji yanakadiriwa kuongezeka kutoka mita za ujazo bilioni 1.829 mwaka 2025 hadi bilioni 2.124 ifikapo mwaka 2030, wakati kiasi cha maji kinachotarajiwa kupatikana mwaka huo ni mita za ujazo bilioni 1.783.
Utafiti huo umeonesha kuwa shughuli za kilimo ndizo zinazotumia sehemu kubwa ya maji katika bonde hilo, zikifuatiwa na ufugaji na matumizi ya majumbani. Aidha, imebainika kuwa mvua nyingi hunyesha kati ya Novemba na Aprili, huku kiwango cha maji katika Mto Bubu kikipungua kati ya Mei na Oktoba, hali inayoweza kuathiri uzalishaji wa mazao, shughuli za ufugaji na upatikanaji wa maji kwa wananchi, hususan katika maeneo ya chini ya bonde.

Katika tathmini ya mwenendo wa baadaye, utafiti umeonesha uwezekano wa kuongezeka kwa vipindi vya mtiririko mkubwa wa maji wakati wa mvua, sambamba na changamoto za uhaba wa maji wakati wa kiangazi. Matokeo hayo pia yamebaini kuwa matumizi makubwa ya maji katika maeneo ya juu ya bonde yanaweza kuathiri upatikanaji wake katika maeneo ya chini, hivyo kuonesha umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi unaozingatia mahitaji ya watumiaji wote, ikiwemo shughuli zinazohusiana na mipango ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa.

                                Kutokana na matokeo hayo, utafiti umependekeza hatua mbalimbali za kujadiliwa na wadau, zikiwemo matumizi ya teknolojia bora za umwagiliaji, uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua, utunzaji wa kingo za mito na maeneo oevu, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika ugawaji wa maji kati ya maeneo ya juu na chini ya bonde. Kupitia warsha hiyo, wadau wamepata fursa ya kujadili gharama za utekelezaji wa mikakati hiyo, usawa katika matumizi ya maji na namna jamii inavyoweza kushiriki katika kulinda rasilimali za maji.
Kwa ujumla, matokeo ya utafiti huo yanatoa tahadhari kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za mapema kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya maji katika Bonde la Mto Bubu. Aidha, yanatarajiwa kusaidia wadau na mamlaka zinazohusika katika kupanga matumizi bora ya maji, kulinda vyanzo vilivyopo na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali hiyo kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.










PICHA NA TATYANA CELESTINE. ZAIDI BOFYA HAPA CHINI

Post a Comment

0 Comments